• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
AFYA: Faida za mananasi katika mwili wa binadamu

AFYA: Faida za mananasi katika mwili wa binadamu

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MWILI unapokosa kinga imara, huwa katika hatari ya kushambuliwa na kila aina ya magonjwa.

Nanasi ni moja kati ya matunda yenye vitamini nyingi na virutubisho vingine vyenye uwezo wa kuupa kinga mwili wako dhidi ya magonjwa.

“Bromelain” ambayo hupatikana kwa wingi kwenye tunda hili, hulifanya liwe muhimu sana katika kujenga na kuimarisha kinga ya mwili.

Ili upate kinga dhidi ya maradhi kwa kula nanasi, unashauriwa kula tunda hilo kabla au baada ya kula mlo wako. Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa lishe husema ni muhimu kula matunda kabla ya mlo mkuu.

Usagaji wa chakula

Nanasi lina virutubisho vinavyouwezesha mfumo wa usagaji chakula tumboni kufanya kazi yake ipasavyo. Mfumo huu unapowezeshwa kufanya kazi yake vizuri, mtu huweza kupata choo laini na kwa wakati kama inavyotakiwa.

Kinga ya mwili

Nanasi linaaminika pia kuwa miongoni mwa matunda yenye Vitamini C kwa wingi ambayo kazi yake ni kuupa mwili kinga dhidi ya “wavamizi” mbalimbali (free radicals), ambao wanapoingia mwilini, kazi yao huwa ni kuharibu chembembe hai za mwili.

Vitamini C inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili. Mwili huwa na uwezo wa kujikinga dhidi ya magonjwa madogomadogo kama vile mafua, kikohozi, homa na maambukizi mengine.

Chanzo cha madini

Mbali ya kuwa ni chanzo kizuri cha vitamini C, nanasi pia ni chanzo kizuri cha madini aina ya ‘Manganese’ ambayo yanaaminika kuwa na uwezo wa kuboresha ufanisi wa vimeng’enyo mbalimbali vya mwili, vikiwemo vya kuzalisha nishati na kinga.

Kuimarisha nuru ya macho

Inawezekana karoti ikawa ndiyo inayojulikana na watu wengi kuwa na uwezo wa kuimarisha nuru ya macho lakini nanasi nalo lina uwezo mkubwa wa kuimarisha nuru ya macho. Ulaji wa tunda hili na matunda mengine, kiasi cha milo mitatu kwa siku, kunaondoa hatari ya kupungua kwa nuru ya macho kwa asilimia 36 kwa watu wazima.

Mara baada ya nanasi kumenywa na kukatwa vipande, linatakiwa kuliwa mara moja, iwapo litahifadhiwa kwenye jokofu kwa ajili ya kuliwa baadaye, njia sahihi ya kuhifadhi ni kuliweka kwenye chombo chenye mfuniko.

Hii husaidia kuhifadhi virutubisho vyake kwa kipindi cha hadi siku tano bila kupoteza ubora wake, ikiwa pamoja na ladha.

Unaweza kula vipande vya nanasi au unywe juisi yake.

Juisi ya nanasi. Picha/ Margaret Maina

You can share this post!

PIC yaamuru ukaguzi wa benki ya NBK huku ikipinga kuuzwa...

BAMBIKA: KFCB bado mpo mtaani?

adminleo