Makala

KILIMO: Wakulima washauriwa kukumbatia mfumo asilia kupunguza asidi udongoni

July 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

MBALI na soko, changamoto zingine katika kilimo ni magonjwa na wadudu wanaovamia mimea na kuharibu mazao.

Baadhi ya wakulima wameishia kuhangaishwa na masuala haya mawili, kilele kikiwa kukadiria hasara chungu nzima na hata wengine kukiasi.

Magonjwa na wadudu, yanapoathiri mimea hushusha kiwango cha mazao. Yanayofanikiwa kuvunwa, ingawa yana udhaifu utokanao na athari hizo hukataliwa sokoni.

Hata hivyo, matumizi ya pembejeo hususan fatalaiza inalimbikiziwa lawama kusaidia kusambaa kwa magonjwa.

Wataalamu wa kilimo wanahoji fatalaiza ikitumika kwa muda mrefu huzidisha kiwango cha asidi udongoni, ambacho hujiri na magonjwa mbalimbali.

“Asidi nyingi udongoni inahusishwa na magonjwa ya mimea. Inasababishwa na utumizi wa fatalaiza kwa muda mrefu, ambapo hata dawa hushindwa kuyadhibiti,” anaonya Bw David Kariuki, mtaalamu na afisa wa kilimo kaunti ya Kirinyaga.

Kulingana na mdau huyu changamoto hii inachangiwa pakubwa na ukodishaji wa mashamba, ambapo wanaokodi hutumia fatalaiza yenye kemikali kuongeza mazao.

“Kwa kuwa lengo ni kupata mazao mengi, anaendelea kuitumia kupita kiasi hadi muda wake utakapokamilika. Hii ni hatari kwa udongo kwani huendelea kuwa dhaifu na kupoteza rutuba. Magonjwa na wadudu yanakuwa vigumu kuangamizwa kwa sababu ya asidi nyingi inayopiku nguvu za dawa,” anafafanua.

Erastus Muriithi ni mkulima wa nyanya Kirinyaga na anasema kuzidi kwa asidi udongoni kumetatiza wengi. Bw Muriithi anasema si mara moja au mbili amekadiria hasara isiyomithilika kwa ajili ya udongo wenye asidi nyingi.

“Nimepoteza mazao yenye thamani zaidi ya milioni kwa sababu ya magonjwa yanayohusishwa na udongo. Ni suala linalozidi kutuhangaisha na tunaomba serikali kupitia sekta ya kilimo iangazie ubora wa mbolea,” anasema.

Ili kutatua hili, mtaalamu David Kariuki anahimiza haja ya kurejelea na kukumbatia mfumo asilia kufanya kilimo. Anasema kuzidi kwa asidi udongoni kutaangaziwa ikiwa wakulima wataitikia kutumia mbolea ya mifugo.

“Asidi si changamoto ya eneo la Kirinyaga pekee, ila ni ya taifa kwa jumla. Ukitumia mbolea asilia mfululizo itashusha kiwango cha asidi kwenye udongo. Pia itapunguza usambaaji wa magonjwa na wadudu,” anashauri Bw Kariuki.

Joseph Gichuki, mtaalamu wa masuala ya udongo anahimiza umuhimu wa mkulima kujua kiwango cha asidi na alkalini cha shamba analonuwia kufanya zaraa kabla kuanzisha shughuli hiyo.

“Utakapopimiwa udongo katika maabara, utashauriwa namna ya kuutibu endapo asidi imepita kiwango kifaacho,” anasema Bw Gichuki.

Aghalabu, mimea mingi hustawi katika udongo wa asidi kati ya pH 6.0-7.5.

Wakulima pia wanahimizwa kutumia pembejeo; mbegu, fatalaiza na dawa dhidi ya magonjwa na wadudu, zilizoidhinishwa na taasisi husika kutathmini ubora wa bidhaa.