Makala

DAU LA MAISHA: Anapigana na desturi potovu kuokoa waseja na hata walioachika

July 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

WAHENGA walisema muacha mila ni mtumwa, msemo ambao umesababisha kuwepo kwa jitihada kibao kuhifadhi baadhi ya tamaduni.

Lakini hata tunaposisitiza umuhimu wa kudumisha baadhi ya itikadi zetu za zamani, ukweli ni kwamba nyingi yazo zimekuwa chanzo cha ukiukaji wa haki za binadamu.

Kwa mfano katika jamii ya Waluo, ni mwiko kwa mwanamke aliyebalehe au kuhitimu umri wa kuolewa na hajaolewa kuzikwa nyumbani alikozaliwa endapo atafariki.

Kulingana na utamaduni wa jamii hii, mwanamke anapofariki katika umri huu na kuzikwa nyumbani kwao, yeye hugeuka na kuwa pepo au kisirani kwa jamii, na endapo hilo litafanyika basi atakuwa kizingiti cha kuzuia wanawake wengine katika familia hiyo kuolewa.

Haya ni kulingana na Roseline Anyango, 46, mkazi wa eneo la Sindo, Mbita, Kaunti ya Homa Bay.

“Mwanamke aliyezidi umri wa miaka 18 akizikwa katika boma la babake, huzuia sio tu wanawake katika boma lake kuolewa, bali katika kijiji kizima. Kutokana na hilona kuambatana na utamaduni wetu, mwanamke wa aina hii huzikwa kwa shangaziye

Endapo hilo haliwezekani, basi mzee yeyote anaweza kujitolea kumzika,” asema.

Ni itikadi za aina hii zilizochochea ari ya Mary Oyier kuanzisha kampeni kali za kupigania haki za wanawake kutoka jamii hiyo ili kuzikwa nyumbani walikozaliwa.

Kupitia mradi wa One Nation Under God, Bi Oyier ananuia kurejeshea wanawake kutoka jamii hii haki ya kuzikwa nyumbani kwao endapo hawataolewa au ndoa zao zitafeli.

“Aidha, utamaduni wa Waluo hauruhusu wasichana kujenga nyumba kwenye ardhi ya baba yao. Wanasema kwamba wanawake ni kama ndege na watapata utulivu tu, walikolewa. Hii inamaanisha kwamba mwanamume akiwa na mabinti pekee, basi wasichana hao kamwe hawatawahi kurithi ardhi.

“Kwa bahati mbaya mwanamke akifa kabla ya ndoa, basi mwili wake utazikwa nyuma ya boma la babake, itikadi ambazo tunapaswa kukabiliana nazo,” aeleza.

Anasema kwamba madhumuni yao ya kupigania haki ya mwanamke kuzikwa kwao sio tu kwa sababu ya kifo, bali ni ili waweze kurithi ardhi ya baba zao, haki ambayo wamenyimwa kwa muda mrefu.

Huku akitoa mfano wa mwanamke fulani aliyelazimika kununua ardhi ya babake na kujenga ili angaa kudumisha chimbuko lake, Bi Oyier anasema kwamba mara nyingi wanawake wanaokumbwa na masaibu haya, hawaruhusiwi kupigania haki zao.

Ni suala ambalo anasema kwamba limewalazimu wengi kutoka jamii hii kukwama katika ndoa na mahusiano mabaya ili kuwa salama na kupata mahali pa kuzikwa, mauti yatakapobisha.

Kuanzisha shirika

Anasema alianzisha shirika hili baada ya ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007 na 2008, akipania kushughulikia masuala ya amani na kuwapa kina mama uwezo wa kifedha.

Lakini mradi huu ambao kwa sasa una wanachama 20, umekuwa pia ukijihusisha na kampeni za kupigania haki ya wanawake kutoka jamii ya Waluo kuzikwa walikozaliwa.

Kulingana naye, kilichochoea zaidi kampeni hizi ni masaibu yanayokumba wanawake katika jamii yake. “Nilishuhudia wengi wakipoteza biashara au wahuni kulipwa kuwashambulia,” asema.

Japo hakuna manufaa yanayotokana na mwanamke kuzikwa kwao, asema, vita hivi vitakabiliana na utamaduni unaowadunisha wanawake, vile vile vitawapa nguvu na usemi wa kujitetea.

Japo kampeni zake hazijashika kasi, anakiri kuwa kibarua kikubwa ni kuwarai wanawake wengine kutoka jamii hii kuungana naye.