Habari Mseto

OCS motoni kumruhusu Itumbi kustarehe seli

July 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MKUU wa kituo cha polisi cha Muthaiga jijini Nairobi (OCS) Alphonse Kimengua amesimamishwa kazi kwa muda kwa kumruhusu mhudumu wa Ikulu Dennis Itumbi kustarehe na marafiki zake ndani ya seli ya kituo hicho.

Picha zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zilimwonyesha Bw Itumbi akiwa pamoja na mtangazaji wa televisheni Jacque Maribe, mwanasiasa Josiah Murigu na kakake David Itumbi wakipiga picha za “selfie” na kushiriki vinywaji ndani ya seli hiyo.

Kulingana na wakuu wa idara ya polisi, maafisa wa polisi katika kituo cha Muthaiga pia walimruhusu Bw Itumbi kupiga gumzo na marafiki zake katika seli hiyo ambako picha hizo zilikuwa zikipigwa.

“Bw Kimengua amechukuliwa hatua hiyo kwa kuruhusu mshukiwa kuburudika na marafiki huku wakipiga picha na kuzituma kwenye mitandao ya kijamii. Hii ni kinyume cha taratibu na kanuni zinafaa kuzingatiwa kwenye seli,” akasema afisa mmoja ambaye aliomba kutotajwa jina.

“Kwa hivyo OCS huyo ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria kwa kufeli kuhakikisha sheria na kanuni za kituo cha polisi zinazingatiwa na washukiwa wote bila ubaguzi,” akaongeza.

Bw Itumbi, ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano ya kidijitali katika Ikulu, anazuiliwa kwa siku tano kufuatia amri ya mahakama ili kutoa nafasi ya kukamilishwa kwa uchunguzi dhidi yake.

Tuhuma

Hii ni baada ya kufikishwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi, mnamo Alhamisi kwa tuhuma za kuandika barua feki iliyodai kulikuwa na njama ya kumuua Naibu Rais William Ruto.

Kulingana na barua hiyo iliyosambazwa mitandaoni, njama hiyo ilikuwa imepangwa na mawaziri wanne kwenye mikutano iliyodaiwa kufanyika katika mkahawa wa La Mada, ulioko kando ya barabara kuu ya Thika.

Mawaziri hao; Peter Munya (Biashara), Sicily Kariuki (Afya), Joe Mucheru (ICT) na James Macharia (Uchukuzi) walikanusha madai hayo baada ya kuamriwa kufika katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Jumatatu wiki jana.

Kukamatwa kwa Bw Itumbi kumepingwa vikali na wabunge wanaoegemea mrengo wa “Team Tangatanga” wanaodai ni njama ya kuwatia woga ili wasiendelea kumpigia debe Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.