• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
‘DARAJA YA MUNGU’: Daraja asili ambalo lingali imara licha ya umaarufu kufifia

‘DARAJA YA MUNGU’: Daraja asili ambalo lingali imara licha ya umaarufu kufifia

Na PHYLLIS MUSASIA

KUTEMBEA kwingi kuona mengi.

Kadri mtu anavyotembea ndivyo anaimarisha kiwango cha ufahamu wa vilivyomo duniani; vya kustaajabisha, kuhuzunisha, lakini muhimu zaidi vya kufurahisha.

Safari ya kutoka Nakuru hadi mtaani Keringet, eneobunge la Kuresoi Kusini lililopo mpakani mwa kaunti ya Nakuru na Kericho inamuacha msafiri na kumbukumbu tele.

Takribani kilomita saba hivi kutoka kwenye barabara kuu inayounganisha eneobunge la Molo na Kuresoi Kusini, kuna kituo cha kibiashara cha Chebara ambapo wamiliki wengi ni wa jamii ya Ogiek.

Hapa, wenyeji wana matumaini kwamba ipo siku serikali ‘itakumbuka’ kijiji chao kwa kuwa na mandhari spesheli; daraja ambalo wanasema limetengezwa kwa ubunifu wa kipekee wa Mwenyezi Mungu.

Mwanya katika sehemu moja ya daraja na ambao hupisha maji ya Mto Chebara. Picha/ Phyllis Musasia

Daraja hilo kwa jina ‘Daraja ya Mungu’ liko kwenye eneo la msitu wa Tinet.

“Nifuate, usiogope. Humu ndani ni salama, hamna wanyama wakali ambao unaweza kohofia kwamba watakudhuru,” ananieleza mmoja wa watu wa jamii ya Ogiek Bw Silas Barkokwet.

Uchochoro kidogo unaweza kumtisha mgeni, lakini mazingira yenyewe ni yenye matunda asilia kwenye mitunda iliyo tele katika eneo hili.

Kwa umbali, macho yanakutana na mlima mkubwa wa mawe.

“Tumekaribia. (Lile) Ile (ndilo) ndiyo ‘Daraja ya Mungu’ ambayo wakazi wa hapa hutumia kuvuka hadi ng’ambo ya pili ya Mto Chebara,” anaeleza Bw Barkokwet.

Hapo mtu anaweza kujisahau kabisa. Maji yanatiririka taratibu huku sauti za nyuni zikisikika pale ndege wanafurahia kazi ya Muumba.

Kulingana na maelezo ya mtumishi huyo wa Mungu, yeye ameishi eneo hilo kwa muda wa zaidi ya miaka 20.

“Nilihamia huku mapema miaka ya tisini (1990s) na wakati huo eneo hili lilikuwa linaenziwa na watu wengi. Ilikuwa kawaida kuwaona wageni – wakiwemo wanafunzi wa shule na raia wa kigeni – wakifika hapa kujionea maajabu ya daraja lenyewe,” anasema Bw Barkokwet.

Aidha anaeleza kwamba eneo hili lilitambulika na hata mpiganiaji wa ukombozi, Shujaa Dedan Kimathi alilipenda mno.

“Dedan Kimathi alitumia eneo hili kama maficho wakati wa vita dhidi ya ukoloni. Kila mara angefika hapa, angekaa vyema bila kutambulika na maadui kule aliko,” anasema.

Daraja hilo lina umbo mithili ya pango na linaweza kuhifadhi watu wajihisi tu ni kama wako kwa nyumba.

Giza totoro

Chini kabisa ya pango hilo ndiko unasikia mtiririko wa maji ya mto Chebara lakini msafiri hawezi kuona maji hayo kwa macho.

Sehemu hiyo nzima ina giza totoro, na kuingia ndani mtu atahitaji mwangaza wa tochi.

Kimathi, kulingana na maelezo, alipenda eneo hilo kwa sababu ya ubora wake ambao alihisi ungemfaa wakati wa kujificha asijekuta na kudhuriwa na maadui.

Hata hivyo, eneo hilo limekuwa likipoteza umaarufu kadri miaka inavyosonga kiasi cha kuanza kusahaulika kabisa.

“Ni watu wachache sana – tena wa kutoka Kuresoi – ndio wanafika eneo hili kujionea na hata kutaka kupumzika. Wageni kutoka nje hatuwaoni tena,” anasema.

Daraja lenyewe lina upana wa takribai mita 30. Unapopita juu yake, huwezi kujua kwamba unapita kwenye daraja kwani ni mlima ambao umetapakaa utadhani ni mlima wa kawaida wa mawe.

Sehemu ya juu ya daraja linalotambulika kama ‘Daraja ya Mungu’. Picha/ Phyllis Musasia

Bw Barkokwet anaeleza kwamba zama zile, jamii ya Ogiek ilitumia pia eneo hilo kufanya tambiko na kuhifadhi vijana wa kiume mara baada ya kupashwa tohara.

Pango la sehemu hiyo ya daraja lilitumika kama makazi ya vijana hao kwa muda wa mwezi mmoja hivi kabla ya wao kutoka jandoni.

Pango katika sehemu moja ya ‘Daraja ya Mungu’. Picha/ Phyllis Musasia

Mgeni anayefika hapa hushangaa namna muda unavyoyoyoma.

Ghafla wanasikika vijana wawili wakiongea tena kwa sauti ya juu ajabu!

Mmoja wao anaasikika akishangaa ni vipi sehemu hiyo imesahaulika licha ya kuvutia macho.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kuzuru huku. Niliambiwa na rafiki yangu kuwa kuna sehemu spesheli eneo hili na nikatamani sana kuja na leo nimefika,” anasema mmoja wao ambaye baadaye anasema anaitwa Vicky. Jina moja tu anataja.

Vicky, akionekana kuwa mwenye umri wa miaka 20 hivi, anasema nia yake kubwa ilikuwa ni kupiga picha akiwa pangoni na pia juu ya daraja hilo.

Wakazi wa Daraja ya Mungu, eneo ambalo lilipata jina kutokana na umaarufu wa kivukio hicho wanasema fahari yao kuu itakuwa kuona sehemu hiyo ikipewa zingatio la serikali ama ya kaunti au serikali kuu ili kurejesha hadhi na sifa kama zamani.

“Tukiwezeza kupigwa jeki na serikali tuna hakika sehemu hii itabadilika na kuvutia watu wengi. Itatuwezesha pia kupata hela za kujimudu kama wakazi wa hapa na pia kuajiri watoto wetu ambao wanakaa bure bila kazi,” anaeleza mwanakijiji mmoja, Bw Josiah Waweru.

You can share this post!

MAPISHI: Scones zilizotiwa juisi ya limau

Raia wa China ashtakiwa kuiba viatu vya mitumba vya Sh3...

adminleo