• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
KINAYA: Dkt Samoei anawahitaji marafiki sampuli hii katika safari ya 2022

KINAYA: Dkt Samoei anawahitaji marafiki sampuli hii katika safari ya 2022

Na DOUGLAS MUTUA

‘SITAKI msaada wako. Hunitakii mazuri!’

Nadhani hayo ndiyo maneno yaliyotoka kinywani mwa Daktari Samoei hivi majuzi alipojua alihadaiwa.

Na nani? Watu waliomdanganya eti kuna kundi la kina mwana wa Mlimani linalokula njama ya kumwondoa duniani.

Hata wewe ukiwa na msaidizi, akae akutungie hadithi kwamba fulani na fulani wanataka kukuua, kisha ujue ni uongo, hapo si ushajua anayetaka ufe nani?

Mbona Dkt Samoei asiwaagize polisi wawashike wakora hao na kuwapeleka mahakamani mara moja, ikibidi wanyimwe dhamana kwa kutishia maisha yake?

Ubunifu, hata kama ni wa kumsaidia mkubwa wako, una viwango.

Kukaa ukaamua kumtia hofu kwa ndoto au hadithi za uongo kuhusu kifo chake ni kujichongea pakubwa.

Anayefanya hivyo ama ana akili ndogo anazotumia kama kofia au hazipo kabisa, ndani ya fuvu mna maziwa ya mgando au ukamasi pekee!

Sasa Dkt Samoei, yule mkali wa siasa na jeuri kutoka Sugoi aliyekizima kimbelembele cha ‘Baba’, anaonekana muoga.

Naam, ndiyo sababu maswali ya kuchekesha kuhusu ujasiri wake Dkt Samoei yameanza kuvuma kotekote mitandaoni.

Juzi mtu wa fitina, mfuasi maarufu wa ‘Baba’, ameuliza mtu atakuwa mwoga kiasi gani ikiwa atajenga nyumba na aogope kuingia.

Nilijibu kimoyomoyo nikasema huyo mtu atakuwa wazimu wa kutupwa na wala si mwoga, yafaa afanyiwe uchunguzi wa akili.

Nani kajenga nyumba kisha akakataa kuingia humo katika muktadha huu? Ni mzaliwa wa Sugoi, aliyesema manoti achangayo kanisani ni ya kujijengea msonge mbinguni.

Mbona basi hataki kwenda huko? Ndivyo maisha yalivyo, hakuna anayetaka kutangulia eti atuache mumu humu tukifurahia utamu wa maisha, hasa ikiwa ana mafedha.

Ukitaka kujua kifo kinavyoogopwa, ingia kwenye kundi la watu wanaosali -na hapa haijalishi dhehebu wala dini- uwaulize ni nani anayetaka kwenda mbinguni.

Kila mmoja atainua mkono na kusema angetaka kuwa wa kwanza kuingia mbinguni ili akaungane na malaika kupasha moto magitaa na magoma kabla wengine hatujafika.

Subiri kidogo watulize kiherehere kisha utoe silaha yoyote, hata ikiwa bandia, uwaambie njia pekee ya kwenda mbinguni ni kufa kwanza, eti watunge foleni uwatume huko!

Mkurupuko na mayowe utakayosikia hapo jamaa wakikimbilia mlangoni na madirishani ili kujinusuru utakuwa wa kupigiwa mfano! Hakuna aliye tayari kwenda mbinguni.

Watu hudai wako tayari kwenda kukutana na Muumba wao wakati ambapo maisha hayawaendei vizuri, si wakiwa na mafedha na familia zenye afya.

Kwa ufupi, nazielewa kelele za mtu mwoga alizopiga Dkt Samoei kutuambia mawaziri wa eneo la Mlimani wanataka kumwangamiza.

Akiambiwa sasa hivi kwamba chumba chake kiko tayari huko mbinguni atasema kitafutiwe mpangaji, ikibidi mmoja wa washindani wake, ili kwanza atuongoze hapo 2022.

Ananikumbusha aliyekuwa mbunge wa Imenti ya Kati, ndugu Gitobu Imanyara, aliyeshurutishwa na wakora kupiga magoti akiangalia Mlima Kenya kisha aseme “Uhuru tuko pamoja” lau sivyo auawe!

Bungeni alieleza alivyowasihi wakora hao wasimuue.

Ajabu, akihadithia hayo alitanua kifua na kusema yuko radhi kufa kwa ajili ya kutetea ukweli. Mwongo!

Hakuna tajiri aliye na haraka ya kuondoka dunia hii! Maisha ya starehe wanayoishi wamwachie nani?

[email protected]

You can share this post!

DINI: Watu wanaangamia kwa kukosa maono, yakujuzu upange...

Madai ya mauaji: Wanajua nini?

adminleo