• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Tangatanga sasa watoa masharti zaidi kwa Rais

Tangatanga sasa watoa masharti zaidi kwa Rais

NA WAANDISHI WETU

VIONGOZI wa chama cha Jubilee wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto wamezidi kumtia presha Rais Uhuru Kenyatta, wakimwekea masharti kadhaa na kudai asipoyatimiza chama hicho kitasambaratika.

Baadhi ya mambo ambayo wanamtaka Rais kufanya ni kuzungumza kuhusu madai ya njama ya kumuua naibu wake, kuwafuta kazi mawaziri waliotajwa, kuitisha mkutano wa chama na kutangaza wazi ikiwa atamuunga mkono naibu wake William Ruto 2022.

Baadhi ya viongozi hao jana waliendelea kukaza kamba kwa Rais avunje baraza lake la mawaziri, huku wengine wakisisitiza kuwa hawatakomesha siasa za 2022.

“Wakenya walitarajia kuwa Rais angewapiga kalamu mawaziri ambao walidaiwa kuhusika katika mpango dhidi ya Naibu Rais, huku uchunguzi ukiendelea,” Gavana wa Nandi Stephen Sang akasema.

Gavana huyo alisema kumekuwa na hali ya taharuki katika baadhi ya maeneo nchini tangu madai hayo yalipoibuka, akisema Rais hafai kuwa kimya.

Wakati huo huo, wabunge Oscar Sudi (Kapseret) na Didmus Barasa (Kiminini) walitishia kuanika kanda ya video ya mkutano ambapo mpango wa kumuua Dkt Ruto uliandaliwa, ikiwa Idara ya Upelelezi(DCI) haitakamilisha uchunguzi huo na kusema kilichoendelea kwa wiki moja.

“Kukamatwa kwa Dennis Itumbi (Mkurugenzi wa mawasiliano ya kidijitali Ikulu) ilikuwa hatua ya kuwahadaa Wakenya tu. Tunataka kuarifiwa kilichofanyika katika hiyo mikutano,” akasema Bw Sudi.

Kando na kuzungumzia suala hilo, Bw Barasa naye alimtaka Rais Kenyatta kutangaza ikiwa bado anamuunga mkono naibu wake, kama alivyoahidi kabla ya uchaguzi wa 2017.

“Ikiwa uliamua kumtupa, tuambie tu tujue tutakavyomfanyia 2022. Huwezi kumtupa naibu wako, ambaye alikusaidia kupata kura nyingi hivyo,” Bw Barasa akasema.

Matamshi yao yalitolewa wakati kiongozi wa wengi Seneti Kipchumba Murkomen, akiwa katika hafla tofauti jana, alimwambia Rais kuwa hawatakomesha siasa za 2022, akisema wanalinda kura za uchaguzi ujao.

Bw Murkomen, ambaye alikuwa katika hafla moja na Dkt Ruto alimwambia Rais Kenyatta kuwa chama si chake peke yake, na kuwa wanatoa amri kwa wananchi, wala si kutoka kwa watu wachache wanaokaa afisini.

“Rais atusamehe, sisi pia tunalinda kura. Jubilee iko na zaidi ya wafuasi milioni nane, ni ngumu watu wawili kutuambia tuache siasa. Tusipoongea siasa za 2022 sasa tutaenda nyumbani na hakuna mtu anayetaka hivyo,” akasema kiongozi huyo, ambaye alikuwa eneo la Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo.

Alisema hivyo, wakati Naibu Rais naye alisisitiza kuwa anataka mambo yote yanayohusu Jubilee kujadiliwa ndani ya chama, badala ya kuanikwa mbele ya umma. Ni matasmhi ambayo alitoa wakati wafuasi wake wamekuwa wakimsukuma Rais kuitisha mkutano wa chama, japo Rais haonekani kutilia maanani suala hilo.

“Yeyote anayejali hii nchi na chama cha Jubilee na umoja ambao ndiyo nguzo yake na mabadiliko ambayo ndiyo msingi wake, hafai kulalamika kuhusu masuala ya chama chetu katika vyombo vya habari kwa misingi ya uvumi, uongo na propaganda, ila katika chama na tutayashughulikia,” Dkt Ruto akasema.

Taarifa ya PETER MBURU, WYCLIFF KIPSANG Na TOM MATOKE

You can share this post!

Wakenya waishangaa CBK kusambaza noti za zamani za Sh1,000

Pendekezo la wabunge kuteuliwa mawaziri lapingwa

adminleo