• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Mirengo ya ‘Embrace’ na ‘Inua Mama’ yakosolewa

Mirengo ya ‘Embrace’ na ‘Inua Mama’ yakosolewa

NA OSCAR KAKAI

VUGUVUGU mbili za viongozi wa kike wa kisiasa za ‘Embrace’ na ‘Inua Mama’ zimekosolewa kwa kuchangia taharuki ya kiasiasa nchini.

Kwa upande mmoja, kikundi cha Embrace huonekana kushabikia handsheki ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, huku kile cha Inua Mama kikihusishwa na kikundi cha Tangatanga kinachoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.

Wakosoaji wa makundi hayo mawili wamesema inasikitisha jinsi viongozi wa kike nao wamejitosa kwenye shughuli zinazotishia umoja wa nchi kupitia makundi hayo.

Wakiongea katika Shule ya Upili ya Paraywa, Kaunti ya Pokot Magharibi, viongozi mbalimbali walionya makundi hayo mawili kuhusu ubabe na malumbano yanayolenga uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Gavana wa kaunti hiyo, Prof John Lonyangapuo na mbunge wa Kapenguria, Bw Samuel Moroto waliwataka viongozi wa kike kutuliza joto la kisiasa na kukoma kuwagawanya Wakenya.

“Kile ambacho tunaona ni kama malumbano ya Ndizi na Machungwa ya mwaka wa 2015. Kina mama ni nguzo ya jamii na wakianza kujiunga kwenye mirengo tunapoteza mwelekeo kama nchi. Vijana na wanasiasa wanaenda kasi. Tunafaa kuheshimu wazee, wapiga kura na watoto. Kina mama wamepotoka,” alisema.

Prof Lonyangapuo alionya dhidi ya kampeni za mapema akiyataka makundi hayo mawili kukomesha siasa na kuhudumia Wakenya kimaendeleo.

“Mbona watu wanafanya mambo ni kama hakuna Rais nchini? Wacha wakumbuke kuwa watachaguliwa kuhusiana na utendakazi wao wala sio mirengo ya kisiasa,” alisema.

Kwa upande wake, Bw Moroto alisema makundi tofauti ambayo yanabuniwa yanachochea taharuki nchini.

“Tumesikia kuhusu watu kulengwa kuuawa na sisi kama wale ambao hutembea na naibu wa Rais lazima tuchukue tahadhari,”alisema Bw Moroto.

Mbunge huyo alisema kuwa watamuomba Mungu ili ukweli uweze kubainika .

Alitoa wito kwa idara ya upelelezi wa jinai (DCI) kutoogopa na kutopendelea upande mmoja kwenye uchunguzi wa madai ya kumuua Dkt Ruto.

Bw Moroto alimtaka Rais Kenyatta kujitokeza wazi na kuitisha mkutano wa baraza la chama cha Jubilee ili kukomesha malumbano ndani ya chama hicho tawala.

You can share this post!

Gavana ajitolea kushauri ‘mbunge mlevi’

Wakulima wazindua kiwanda cha kahawa cha Sh4m

adminleo