Kenya yadumisha nafasi yake kwenye kamati ya Wake wa Marais Afrika
CHARLES WASONGA na PSCU
KENYA Jumatatu ilidumisha wadhifa wake kwenye kamati shikilizi ya Shirika la Maendeleo la Wake wa Marais, (OAFLAD) kwa kipindi cha miaka miwili kuwakilisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa mara ya tatu.
Kongamano la 23 la Shirika la OAFLAD lililosimamiwa kwa pamoja na Mke wa Rais, Uhuru Kenyatta, Bi Margaret Kenyatta na Mke wa Rais wa Burkina Faso Sika Bella Kaboré pia ulipendekeza Rwanda na Burundi kama wakikilishi wengine wa Afrika Mashariki.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itawakilisha kuwakilisha kanda ya Afrika ya kati huku Msumbiji na Namibia zikiwakilisha Afrika ya Kusini.
Nazo Niger na Sierra Leone zitawakilisha Afrika Magharibi. Wanachama wa kamati shikilizi huendesha na kusimamia majukumu ya shirika hilo.
Wanawakilisha shirika la OAFLAD na kuhakikisha linaimarika katika maeneo yao mbali mbali. Kamati shikilizi vile vile ina majukumu ya kutekeleza maazimio ya Kongamano kuu.
Mkutano huo ulifanyika jijini Niamey, nchini Niger pia ulishuhudia kuchaguliwa kwa Mke wa Rais wa Congo Brazavilee Bi Antoinette Sassou Nguesso kuwa Rais mpya wa shirika la OAFLAD.
Alichukua hatamu za uongozi kutoka kwa Mke wa Rais wa Burkina Faso Sika Bella Kaboré
Kwa upande wake Bi Kenyatta alikabidhi wadhifa wa Naibu Rais kwa Mke wa Rais wa Zimbabwe Auxilia Mnangagwa.
Maudhui ya Kongamano Kuu la 23 la shirika la OAFLAD ni ‘Kushirikiana Kubadilisha Afrika na Kushughulikia Mahitaji ya Watu wanaokabiliwa na Hatari.
Ili kuimarisha shughuli na utendakazi wa Shirika la OAFLAD, wake hao wa Marais wa Afrika waliidhinisha mikakati kuhusiana na ukusanyaji wa malimbikizi ya fedha za uanachama sharti itekelezwe kikamilifu kuimarisha uwezo wa kifedha wa shirika hilo.
Awali, shirika hilo la wake wa marais wa mataifa ya Afrika lilijulikana kama Shirika la Wake wa Marais dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi (OAFLA). Lengo lake lilikuwa kutoa sauti yenye umoja kutetea makundi yanayoishi au yaliyoathirika na ugonjwa wa Ukimwi na virusi visababishao ugonjwa huo (HIV).
Liligeuza jina kuwa OAFLAD mapema mwaka huu, na kupanua kazi zake ili kushirikisha masuala mengine ya maendeleo yanayoathiri bara hili yakiwepo magonjwa ya kuambukizwa, usawa wa kijinsia, kuwapa uwezo wanawake na vijana, afya ya akina mama na watoto miongoni mwa masuala mengine yanayoathiri maendeleo.
Wake wa Marais Aïssata Issoufou Mahamadou (Niger), Fatima Maada Bio (Sierra Leon), Monica Geingos (Namibia), Keïta Aminata Maiga (Mali), Hinda Déby Itno (Chad) na Isaura Nyusi (Msumbiji) ni baadhi ya waliohudhuria mkutano huo.
Kongamano hilo la OAFLAD lilifanyika pembezoni mwa Kikao Maalum cha 12 cha Marais na Viongozi wa Mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri, ambaye ndiye Mwenyekiti wa umoja huo, alifungua kongamano hilo ambalo litajadili utekelezaji wa mkataba wa Maeneo ya Biashara Huru Barani Afrika (AFCFTA).
Rais Sisi alisisitiza kwamba kuzinduliwa kwa mkataba huo kunaashiria ufanisi muhimu wa Afrika, akiongeza kwamba kundi hilo la kiuchumi litasaidia kufungua uwezo wa kiuchumi wa bara hili.
Hii itafanyika kupitia uimaeishaji wa biashara kati ya mataifa ya Afrika, kuboresha mifumo ya utoaji na utengenezaji bidháa na kusambaza ujuzi.