Wageni kusimamia eneo jipya la mizigo bandari ya Mombasa
NA ANTHONY KITIMO
SERIKALI Jumatatu ilikabidhi rasmi kampuni ya kigeni ya Mediterranean Shipping Company (MSC) usimamizi wa sehemu ya mizigo ya Bandari ya Mombasa licha ya pingamizi kutoka kwa wabunge na wafadhili wa mradi huo.
Rais Uhuru Kenyatta aliongoza utiaji saini wa usimamizi huo licha ya wabunge wa Pwani wakiongozwa na Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir kupinga vikali pendekezo hilo bungeni.
Wiki iliyopita balozi wa Japan, ambayo ilifadhili mradi huo, na wenzake wa Ufaransa na Uingereza walipinga mapendekezo hayo ya kubinafsisha sehemu hiyo ya bandari.
Mabalozi hao walisema ikiwa serikali ya Kenya ilifaa kutangaza tenda ya usimamizi huo ili kampuni zingine zitume maombi kama ilivyokuwa katika mkataba wa kufadhili wa mradi huo unaofahamika kama Container Terminal 2 (CT2).
Sehemu hiyo ya mizigo ambayo imekuwa ikozozaniwa ni mojawapo ambayo serikali imewekeza mabilioni ya pesa, na inatajwa kuwa ya kisasa kwani inapokea zaidi ya asilimia 45 ya mizigo yote inayoingia na kutoka bandarini.
CT2 pia imeunganishwa na reli ya kisasa (SGR) na kwa sasa mradi wa kupanua sehemu hiyo ya mizigo unaendelea kukamilishwa, hivyo kuhakikisha itakuwa ikichukua sehemu kubwa ya mizigo katika Bandari ya Mombasa.
Akiongoza ukabidhi huo kwa MSC, Rais Kenyatta alisema kampuni hiyo itashirikiana na Kenya National Shipping Line kusimamia CT2 iliyojengwa kwa gharama Sh27 bilioni.
“Ningependa kuwapongeza wabunge kwa kupitisha sheria ambazo zitaleta maendeleo nchini na kwa miaka 10 ijayo tunanuia kuongeza biashara katika bandari ya Mombasa kwani kampuni ya MSC itawezesha kuboresha sio tu mizigo inayoingia nchini bali pia itaboresha utalii,” alisema Rais Kenyatta.
Katika mkataba wa pili uliotiwa sahihi hapo jana, Chuo cha Ubaharia na Ufundi kitashirikiana na MSC kutoa mafunzo kwa wanafunzi hao ambao hulazimika kusafiri hadi jiji la Dar es Salam kupata mafunzo ya ubaharia.
Chuo hicho kitaanza kutoa mafunzo maalum kwa wafanyikazi wa MSC, jambo ambalo limevutia wakazi wengi.
Wakati huo huo, sehemu ya wafanyikazi katika chuo hicho wameomba serikali kutoa suluhisho kwa matatizo yao baada ya kitengo hicho kuhamishwa kutoka Halmashauri ya Bandari (KPA) hadi Halmashauri ya Masuala ya Bahari nchini (KMA).
Wafanyikazi hao walidai kuwa masuala yao yao uajiri yametelekezwa tangu mikakati ya kubadilisha kitengo hicho kuanza.