• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
AUNTY POLLY: Nitajuaje ikiwa ana maradhi ya zinaa?

AUNTY POLLY: Nitajuaje ikiwa ana maradhi ya zinaa?

Na PAULINE ONGAJI

MIMI ni mwanafunzi wa kike ambaye yuko katika chuo kikuu. Nina mpenzi niliyekutana naye chuoni miezi kadha iliyopita. Amenizidi umri na anatarajiwa kukamilisha elimu ya shahada yake chuoni mwaka huu. Hata hivyo, katika siku za hivi majuzi, amekuwa akinishinikiza tushiriki mapenzi. Yeye ni maarufu sana na najua kwamba wasichana wengi wanammezea mate; suala linalonifanya nipate msukumo wa kutimiza ombi lake. Hata hivyo, naogopa kwani najua kwamba ana wapenzi wengi chuoni na nje; wasichana ambao nina uhakika kwamba yeye hushiriki mapenzi nao. Nitatambuaje iwapo ameambukizwa maradhi ya zinaa katika shughuli zake hizi za ukware?

Emma, 20, Nairobi

Kwanza ningependa kujua umejua vipi kwamba amekuwa akishiriki ngono kiholela? Ikiwa yeye mwenyewe amekueleza ukweli kuhusu mahusiano yake ya awali, hiyo ni ishara kwamba kwa kiwango fulani anaaminika na hivyo anakupenda. Lakini hiyo sio sababu tosha ya kuhatarisha afya yako kwa kulala na mtu usiyejua hali yake ya kiafya.

Hata hivyo, huwezi kujua mtu anaugua maradhi ya zinaa kwa kumwangalia tu. Wakati mwingine hata watu wanaougua maradhi ya zinaa hawafahamu kuwa ni wagonjwa. Hatua ya kwanza ni nyote kupimwa kubaini ikiwa mna maradhi yoyote ya zinaa.

Kondomu ndiyo njia bora ya kuzuia mimba na maradhi ya zinaa na hivyo ikiwa unahisi kana kwamba uko tayari kuchukua hatua hii, hakikisha kuwa unatumia vyema kinga kila mara. Muhimu kujua ni kuwa kondomu haikuhakikishii usalama kabisa, na ndio sababu lazima umhusishe mwenzio kwa kuzungumza naye kabla ya kushiriki ngono.

Ikiwa umewahi kushiriki ngono awali, wewe na mwenzio mwaweza andamana kwenye kituo cha kiafya na kupimwa pamoja. Mkiwa hapo ulizia kuhusu mbinu za upangaji uzazi kwani kuna uwezekano wa kushika mimba hata ukitumia kinga hasa ikiwa hamtumii jinsi inavyofaa.

Zaidi ya yote ningependa kukufahamisha kwamba kushiriki mahaba ni hatua kubwa maishani kwani kuna hatari ya maambukizi ya zinaa, kushika mimba, au vyote viwili, suala ambalo bila shaka lina uwezo wa kubadilisha maisha yako.

Unapaswa kuchukua hatua hii na mtu unayempenda na ambaye mnaaminiana kwani hata baada ya kupimwa, ikiwa kwa kweli anajihusisha na mahusiano mengine, anahatarisha maisha yake na yako.

You can share this post!

MAPOZI: Nviiri

UNABISHA? Madagascar na Algeria ni ramba mtu tu AFCON

adminleo