• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
UNABISHA? Madagascar na Algeria ni ramba mtu tu AFCON

UNABISHA? Madagascar na Algeria ni ramba mtu tu AFCON

Na MASHIRIKA

CAIRO, Misri

MADAGASCAR iliendelea kudhihirishia ulimwengu haiko nchini Misri kutalii, bali kushindania taji la Kombe la Afrika (AFCON) baada ya kunyamazisha washindi wa mwaka 1968 na 1974 DR Congo kwa njia ya penalti 4-2 na kutinga hatua ya robo-fainali mjini Alexandria, Jumapili.

Katika usiku mmoja ambao pia mabingwa wa mwaka 1990 Algeria walijikatia tiketi ya robo-fainali kwa kuaibisha Guinea 3-0, washiriki wapya kabisa Madagascar walisumbua vijana wa Florent Ibenge kuanzia kipenga cha kwanza kabla ya kuwafundisha jinsi ya kupiga penalti baada ya muda wa kawaida na ule wa ziada kutamatika mabao yakiwa 2-2.

Ibrahim Amada aliwapa wanavisiwa hao bao la ufunguzi dakika ya tisa liliamsha Leopards, ambayo ilisawazisha 1-1 dakika ya 21.

Hata hivyo, Faneva Andriatsima alirejesha Barea mbele 2-1 alipotikisa nyavu dakika ya 77.

Madagascar iliona ushindi ukiiponyoka dakika ya 90 pale Chancel Mbemba alipopata bao la pili la DR Congo na kulazimisha dakika 30 za ziada kusakatwa.

Amada alianzishia timu yake vizuri katika upigaji wa penalti, huku DR Congo ikipata pigo baada ya Marcel Tisserand kupoteza.

Romain Metanire, Thomas Fontaine na Jerome Mombris walifungia Madagascar penalti zilizofuata nayo DR Congo ikaongeza mbili kupitia kwa Cedric Bakambu na M’Poku Ebunge kabla ya Tisserand kupoteza yake na kuipa Madagascar ushindi.

Kabla ya ushindi huo muhimu, Madagascar, ambayo inanolewa na Mfaransa Nicolas Dupuis, ilikuwa imetuma onyo kwa wapinzani kwa kuduwaza Super Eagles ya Nigeria 2-0 katika mechi yake ya mwisho ya makundi.

Madagascar itamenyana na Tunisia katika robo-fainali mnamo Julai 11.

Carthage Eagles ya Tunisia ilipiga Black Stars ya Ghana 5-4 katika penalti baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 katika muda wa kawaida na wa ziada Jumatatu usiku.

Mechi kati ya Madagascar na DR Congo ilifuatiwa na ile kati ya Desert Foxes ya Algeria na Syli Nationale ya Guinea jijini Cairo.

Algeria ya kocha Djamel Belmadi ilizaba Guinea 3-0 kupitia kwa Youcef Belaili, nyota wa Manchester City Riyad Mahrez na Adam Ounas.

Winga Mahrez, ambaye ni mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2016, alisema timu yake iliridhika na matokeo hayo.

“Nadhani tulikuwa na mechi nzuri dhidi ya timu nzuri kutoka Guinea. Hatukufungwa bao na tulipata matatu,” alisema Mahrez.

Kuridhika

“Ulikuwa usiku mzuri sana kwetu na tumeridhika kushinda timu ambayo haikuwa rahisi.”

Huku wenyeji Misri pamoja na mabingwa wa mwaka 1976 Morocco wakiwa wameaibishwa na Afrika Kusini na Benin katika raundi ya 16-bora mtawalia, watu wengi sasa wanapigia upatu Algeria kufika fainali na kubeba taji.

Algeria ndiyo timu pekee ambayo imeshinda mechi zake zote baada ya kulima Kenya 2-0, Senegal 1-0 na Tanzania 3-0 katika mechi za makundi kabla ya kunyoa Guinea bila maji.

Wachezaji wa Algeria washerehekea baada ya kushinda mchuano wa hatua ya 16-bora dhidi ya Guinea katika kipute cha AFCON 2019. Picha/ AFP

Vijana wa Belmadi wanasubiri mshindi kati ya Ivory Coast na Mali katika robo-fainali itakayochezewa mjini Suez. Waalgeria wakipita robo-fainali, watamenyana na mshindi kati ya Nigeria na Afrika Kusini katika fainali Julai 19.

Belmadi alifanya mabadiliko tisa kutoka timu ilionyuka Tanzania katika mechi ya mwisho ya makundi, akirejesha wachezaji wengi wa timu ya kwanza kama Mahrez.

Kwa upande wake, Guinea ilikosa huduma za kiungo wa Liveropool Naby Keita aliyerejea mkekani baada ya kuumia kinena dhidi ya Barcelona mwezi Mei.

Refa alikuwa na kazi ngumu katika dakika 14 za kwanza pale wachezaji walichezeana visvyo akiwaonyesha Mady Camara (Guinea) na Adlene Guedioura (Algeria) kadi ya njano kabla ya Belaili kufungua ukurasa wa magoli dakika ya 24.

Mahrez na Ounas walizamisha chombo cha Guinea kabisa walipopachika mabao dakika ya 57 na 82 mtawalia.

You can share this post!

AUNTY POLLY: Nitajuaje ikiwa ana maradhi ya zinaa?

Vipusa wa USA watetea ubingwa wa Dunia gozini

adminleo