• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
Vipusa wa USA watetea ubingwa wa Dunia gozini

Vipusa wa USA watetea ubingwa wa Dunia gozini

Na MASHIRIKA

LYON, UFARANSA

VIPUSA wa timu ya taifa ya Amerika walitawazwa mabingwa wa dunia kwa mara ya nne katika historia ya kipute hicho baada ya kuwachabanga Uholanzi 2-0 katika fainali iliyowakutanisha jijini Lyon, Ufaransa mnamo Jumapili.

Penalti ya Megan Rapinoe na bao la Rose Lavelle katika kipindi cha pili liliwapa Amerika ushindi uliowasaidia kutetea kwa mafanikio umalkia wa Kombe la Dunia baada ya Uholanzi kuzuia na kuibana sana ngome yao katika dakika 45 za mwanzo wa mchezo.

Winga Rapinoe aliwafungulia Amerika ukurasa wa mabao kupitia penalti baada ya refa Stephanie Frappart wa Ufaransa kurejelea teknolojia ya video ya VAR.

Penalti hiyo ilichangiwa na tukio la beki wa Barcelona Stefanie van der Gragt kumchezea visivyo mvamizi wa USA, Alex Morgan.

Uholanzi ambao ni mabingwa wa bara Ulaya, walikuwa wakishiriki fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya pili katika historia ya kivumbi hiki.

Chini ya ulinzi mkali wa kipa Sari van Veenendaal aliyefanya kazi nyingi za ziada, Uholanzi walifanikiwa kuwadhibiti vilivyo wapinzani wao katika kipindi cha kwanza na kuwanyima nafasi nyingi za wazi.

USA ambao walikuwa wakinogesha fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo, waliendeleza ubabe wao katika jukwaa la kimataifa baada ya kutawazwa mabingwa mnamo 1991, 1999 na 2015.

Bao la Rapinoe pia lilimaanisha kwamba aliibuka Mfungaji Bora wa fainali za mwaka huu baada ya kupachika wavuni jumla ya mabao sita na kuchangia mengine matatu.

Fowadi huyo aliwabwaga Patricia Morgan (USA) na Ellen White wa Uingereza.

Rapinoe vilevile alitawazwa Mchezaji Bora wa kivumbi hicho.

Ufanisi wa USA ulimshuhudia kocha wao mzawa wa Hampshire Uingereza, Jill Ellis akiingia katika mabuku ya historia kwa kuwa mkufunzi wa kwanza kunyanyua ubingwa wa Kombe la Dunia mara mbili mfululizo.

Kulingana na Ellis, ushindi wao wa pili mfululizo ulikuwa mgumu zaidi hasa ikizingatiwa ubora wa kila kikosi katika orodha ya mataifa 24 yaliyoshiriki vita vya kuwania ubingwa wa kipute hicho mwaka 2019.

Amerika yaipiga Thailand 13-0

Katika safari yao ya ufanisi, USA walianza kampeni za Kombe la Dunia kwa matao ya juu baada ya kuwaponda Thailand 13-0 katika ushindi ulioweka historia kwa kuwa mnono zaidi kuwahi kusajiliwa katika fainali za Kombe la Dunia.

Baadaye, kikosi hicho kiliwabwaga Chile na Uswidi kabla ya kuibuka na ushindi wa 2-1 mara tatu dhidi ya Uhispania, wenyeji Ufaransa na Uingereza mtawalia.

Katika fainali za 2015 zilizoandaliwa Canada, USA walivuna ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Japan chini ya dakika 16 za ufunguzi wa kipindi cha kwanza.

Mabao matatu kutoka kwa nahodha Carli Lloyd yaliwasaidia kuwabwaga wapinzani wao hao kwa jumla ya magoli 5-2 hatimaye.

Ingawa hivyo, hali ilikuwa tofauti sana mara hii hasa ikizingatiwa uthabiti wa kikosi cha Uholanzi.

Ushindi wa USA uliwafanya kuwa kikosi cha pili baada ya Ujerumani mnamo 2007 kuwahi kutetea kwa mafanikio ubingwa wa Kombe la Dunia.

You can share this post!

UNABISHA? Madagascar na Algeria ni ramba mtu tu AFCON

Mtihani mkali wawasubiri Chipu katika raga ya dunia

adminleo