KILIMO: Njia bora ya kuandaa kitalu
Na SAMMY WAWERU
MICHE hupandwa kwenye kitalu na kutunzwa hadi ikomae kwa uhamisho shambani.
Mimea kama kabichi, spinachi, sukuma wiki, mboga za kienyeji kama mchicha na mnavu, na nyanya huhitaji miche.
Wataalamu wa kilimo wanasema ufanisi katika uzalishaji wa mazao unategemea miche.
“Pia ni muhimu mkulima kuzingatia mbegu kwani kuna zile bandia sokoni. Mazao bora yanategemea ubora wa mbegu,” ahimiza Emmah Mwenda, kutoka H.M Clause
H.M Clause ni kampuni inayozalisha mbegu na ambayo imeendesha shughuli hiyo kwa zaidi ya miaka 200. Ina matawi yake mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Kitalu kinapaswa kuandaliwa kwa kukiinua kwa udongo karibu mita moja juu kutoka ardhini. Timothy Mburu ambaye mbali na kuwa mkulima wa aina yake eneo la Naromoru, kaunti ya Nyeri, pia ni mtaalamu wa masuala ya kilimo na anasema udongo unapaswa kufanywa laini na mwororo.
Anasema kitalu kitengenezwe kwa makundi, maarufu kama ‘Beds’ kwa Kiingereza.
“Upana huandaa karibu mita mbili, urefu ni kwa mujibu wa kiasi cha miche unayopania kupanda,” anaeleza Bw Mburu.
Kulingana na mkulima huyu ni kwamba udongo unapaswa kuchanganywa sawasawa na mbolea.
Aidha, Mburu amekumbatia mfumo wa kilimo asilia kwa kutumia mbolea hai, vunde au mboji (compost manure).
Hii ni mbolea iliyoundwa kwa kuchanganya kinyesi cha mifugo au kuku na majani na matawi ya mimea na hata miti.
Mkulima huyu anaendelea kueleza kwamba udongo unapochanganywa na mbolea, maji yamwagwe kwa kipimo.
Hatua hii kulingana na Bw Mburu ni kwamba husaidia mchanganyiko huo kuwa laini na mwororo, ambapo hupewa siku moja.
“Andaa mitaro yenye urefu wa sentimita moja kuenda chini, na iwe na nafasi ya nusu futi kutoka mmoja hadi mwingine. Mwaga mbegu kwa utaratibu, kisha ufunike kwa udongo kiasi. Ili kuzuia kufukuliwa na ndege na uvukizi wa maji, kifunike kwa nyasi,” Bw Mburu anafafanua.
Anaongeza kusema kwamba maji yawe yakimwagiliwe asubuhi na jioni, kwa kipimo.
Wakati wa mahojiano kuhusu maandalizi ya kitalu, Meshack Wachira, mtaalamu wa kilimo, alisema nyasi zinapaswa kutumika ni zilizokauka.
“Nyasi mbichi husambaza magonjwa na wadudu,” akaonya mdau huyo.
Mbegu huchipuka kati ya siku 5 hadi 7. Bw Wachira anasema miche itunzwe vyema kwa maji, mkulima akishauriwa kuwa makini kudhibiti magonjwa na wadudu. Ili kuinawirisha, mbolea ya kisasa na isiyo na kemikali inaweza kutumika (top dressing).
“Ikumbukwe miche dhabiti na yenye nguvu huchangia pakubwa katika mazao mengi na bora,” asisitiza Bw Wachira. Miche huwa tayari baada ya siku 30, wiki nne.
Kati ya wakati huo, mkulima anahimizwa kuandaa shamba itakapopandwa. Unapaswa kumwagilia kitalu maji kabla ya kuing’oa. Aidha, unashauriwa kufanya shughuli hiyo majira ya jioni, jua likitua ili kuepuka miale kali.