KAULI YA MATUNDURA: Kila binadamu ana upekee ambao hauwezi kujazwa na mtu mwingine
Na BITUGI MATUNDURA
NILIPOKUWA mwanafunzi wa shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Maseno mnamo miaka ya 1990, mwalimu wangu wa somo la falsafa – Prof Crispin Iteyo aliniambia kauli muhimu ambayo uzito wake unaendelea kunishughulisha na kunifikirisha kadri miaka inavyozidi kusonga na umri wangu kuporomoshwa na wimbi la wakati.
Mwalimu Iteyo alisema kwamba, “Tupende tusipende, lazima tujishughulishe na masuala ya kifalsafa.”
Kadhalika, Prof Iteyo alitugutua kwamba maisha ni mzunguko; ambapo vizazi hupokezana mwenge wa maisha. Pindi mtu anapozaliwa, moyo wake huwa kana kwamba umetiwa majira mithili ya saa.
Hatima ya maisha ya binadamu aijuaye ni Mungu – ila binadamu yule aghalabu huwa ana uwezo wa kuamua mkondo ambao maisha yake yatachukua kutokana na matendo yake ulimwenguni au maamuzi atakayoyafanya. Vivyo hivyo hatuwezi kutilia upofu dhana ya ujaala katika maisha.
Mwalimu na rafiki yangu – Bw Crispine Isaboke ambaye anafundisha somo la falsafa katika Chuo Kikuu cha Chuka ana mtazamo kwamba binadamu hana uwezo wa kudhibiti mkondo ambao maisha yake huchukua.
Anadai kwamba ikiwa mtu fulani ameamua kusafiri kwa ndege kwenda Amerika, uamuzi huo si wake bali ni ujaala.
Ilikuwa imepangwa hivyo.
Mtu huyo akighairi na kuvunja safari, hatua hiyo ilikuwa imepangwa hivyo.
Mawazo ya Bw Isaboke yanaturudisha palepale kwenye udhanaishi (existentialism).
Mwandishi wa fasihi ya Kiswahili ambaye ameegemeza takribani tungo zake zote katika mkabala huu wa udhanaishi ni Euphrase Kezilahabi.
Tatizo la maisha ya mwanadamu linamshughulisha mno Euphrase Kezilahabi katika maandishi yake yote ya kubuni: ‘Kichomi’, ‘Rosa Mistika’, ‘Kichwamaji’, ‘Dunia Uwanja wa Fujo’, ‘Nagona’, ‘Mzingile’ na ‘Dhifa’.
Kezilahabi anamwangalia mwanadamu katika viwango na awamu mbili.
Kwanza, anayahakiki maisha ya mwanadamu katika kiwango cha ubinafsi – yaani mtu binafsi na pili, amamhakiki mwanadamu huyohuyo katika mtagusano wake na watu wengine – yaani jamii.
Kiunzi kikuu kinachofungamanisha tungo za Kezilahabi ni kwamba binadamu huyu – awe katika kiwango cha ubinafsi au jamii pana, anajaribu kutafuta uhuru, furaha, kuusaka ukweli au hata kudadisidadisi iwapo Mungu yupo.
Kwa ujumla, binadamu anajaribu kujiuliza – maisha ni kitu gani? Licha kwamba maswali haya yote ni ya kifalsafa, mtazamo wangu ni kwamba kila binadamu ana nafasi yake muhimu katika dunia hii.
Kwamba kila binadamu amakirimiwa upekee wa namna fulani ambao ni vigumu kuuiga au kuurudufu kwa njia moja au nyingine.
Juha Kalulu
Mfano nitakaoutoa kushadidia upekee wa kila binadamu ni kuhusu mchoraji wa vibonzo vya Juha Kalulu – Edward Gicheri Gitau ambaye aliaga dunia mwaka 2016.
Tangu afariki, hakuna mtu mwingine ambaye amejitokeza kuendeleza kipawa chake cha kuchora vibonzo vya Juha Kalulu kwa mtindo na namna sawa alivyokuwa anachora Mzee Gitau.
Vivyo hivyo, mwandishi mcheshi Wahome Mutahi alipofariki, hakuna mtu aliyeweza kuandika makala ya The Whispers kwa namna na mtindo ule ule alioutumia mwandishi asilia.
Kwa hiyo, sikosei kudai kwamba kila binadamu katika ulimwengu huu anaweza kumtihilishwa na sura mahsusi kwenye jitabu liitwalo maisha.
Unapozaliwa, kuna kitu fulani na upekee wa namna fulani unaouletwa katika dunia hii, na unapofariki, upekee ule hauwezi kufidiwa na mtu yeyote yule.
Kwa hiyo, kila binadamu ana nafasi muhimu katika ulimwengu huu – na anapaswa kutambuliwa na kupewa nafasi ya kuicheza ngoma yake kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Bitugi Matundura ni mtunzi wa riwaya ya ‘Kivuli cha Sakawa’