Mbinu za kukabiliana na ugaidi kufunzwa shuleni nchini Kenya
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta ametangaza kuwa serikali itaanzisha mpango wa kutoa mafunzo kuhusu mbinu za kuzuia ugaidi katika shule za humu nchini baada ya miezi michache ijayo.
Akiongea Jumatano alipofungua rasmi kongamano kuhusu mipango ya kukabiliana na ugaidi katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Mazingira (UNEP), Gigiri, Nairobi, Rais Kenyatta amesema mtaala wa mafunzo ya hayo na fani nyinginezo za usalama wa wanafunzi tayari umetayarishwa na Wizara ya Elimu.
“Lengo kuu la mpango huu ni kuwalinda watoto wetu dhidi ya vitisho vya ugaidi katika maisha yao. Pia masomo aina hiyo yatawakinga kutokana na uwezekano wa wao kusajiliwa kwa mafunzo ya kigaidi,” akasema.
Kumekuwa na visa vingi vya wanafunzi wa shule na vyuo vikuu na vile vya kadri kushawishiwa na wafuasi wa makundi ya kigaidi kwenda kupewa mafunzo ya kigaidi hasa katika taifa jirani la Somalia.
Ni vijana kama hawa ambao hutumiwa na wakuu wa wanamgambo hao wa al-Shabaab kupanga mashambulio ya kigaidi katika maeneo mbalimbali nchini hasa Kaskazini Mashariki na Pwani ya Kenya.
Mkakati
Rais Kenyatta aliongeza kuwa serikali imeandaa mkakati wa kupambana na ugaidi katika ngazi za kaunti kwa lengo la kupunguza visa vya mashambulio na kuimarisha usalama nchini.
“Vita dhidi ya ugaidi za vimegatuliwa kupitia kuandaliwa kwa Mipango ya Kuzuia Mashambulio katika ngazi ya Kaunti,” akasema.
Akaongeza: “Mipango imeundwa ili kuafiki mahitaji ya kila moja ya kaunti 47 na yanashirikisha vikosi vya usalama, maafisa wa utawala, makundi ya mashirika ya kijamaa na wananchi wa kawaida. Lengo hapa ni kutekeleza mipango hiyo katika muda maalumu.”
Rais Kenyatta amesema mataifa ya Afrika yanahitaji kuwa na mikakati thabiti ya kukabiliana na ugaidi na pia kuweka mipango ya kuwasitisha, kuwarekebisha na kuwarudisha katika jamii wale wanaokuwa na mawazo na mafunzo ya kigaidi.
Rais aliongeza kwamba ugaidi ni changamoto kwa Afrika na hivyo basi sharti Afrika ibuni suluhisho na mikakati ya pamoja dhidi ya uovu huo.
“Natoa wito kwa Umoja wa Afrika (AU) kuweka mkataba wa kisiasa wenye nguvu kukabiliana na kushinda ugaidi na namna zote za misimamo mikali yenye kusababisha ugaidi,” akasema Rais.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema Umoja wa Mataifa umejitolea kikamilifu kufanya kazi na mataifa na mashirika yote katika vita dhidi ya ugaidi.
Shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa AU Moussa Faki Mahamat.