• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
Taasisi ya Matric yafungwa mjini Thika

Taasisi ya Matric yafungwa mjini Thika

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO cha Matric Institute of Professional Studies, ambacho kimekuwa kikitoa mafunzo kuhusu maswala ya lishe bora na maankuli mjini Thika, kimefungwa mara moja kwa kukosa kufuata viwango vya ubora vinavyostahili.

Mkurugenzi mkuu wa ukaguzi wa Kenya Nutritionist and Dietician Institute, Bw David Okeyo, amesema waliafikia hatua hiyo baada ya kupata makosa mengine ambayo yalikosa kufuatwa ipasavyo.

Ilidaiwa kuwa wazazi, walimu wenyewe wa chuo hicho na wanafunzi waliwasilisha malalamiko yao baada ya kugundua ya kwamba chuo hicho cha Matrick Institute of Professional Studies kilikosa kufuata sheria zinazostahili kuwekwa ili kuendesha chuo kama hicho.

“Mimi mkurugenzi wa Kenya Nutritionist and Dietician Institute, nilipata malalamishi mengine kuhusu chuo cha Matrick Institute na baada ya kusikiliza lalama niliamua kuchunguza,” alisema Bw David Okeyo.

Kulingana na Okeyo, chuo hicho kinaendeshwa katika makazi ya watu, na kwa hivyo wanafunzi hawapati nafasi nzuri ya kusoma.

Wakati huo pia inadaiwa kuwa walimu katika chuo hicho wanalipwa mshahara duni wa Sh13,000 pekee kila mwisho wa mwezi.

Wakati huo pia ilidaiwa kuwa maabara wananazotumia kwa masomo yao ni za hali ya chini na hazijafika kiwango kinachofaa.

“Hatuwezi kubali wazazi wapoteze fedha zao bure huku wakitarajia wana wao kufanya vyema masomoni. Sheria ni sharti ifuatwe vilivyo,” amesema Bw Okeyo.

Ameamuru wanafunzi wote wa chuo hicho waondolewe hapo Mara moja na kupelekwa katika vyuo vingine vinavyotambulika kirasmi na serikali.

“Tutaendelea kuzuru miji mengine kama Eldoret na Nakuru ambayo pia tunashuku kuna vyuo vya aina hiyo,” amesema Bw Okeyo.

Amewashauri wazazi wawe macho wakati wowote wanapokwenda kuwatafutia wana wao nafasi za vyuo vya mafunzo.

“Iwapo watawatafutia vyuo vingine watalazimika kulipia karo upya. Tunajua in gharama lakini ndivyo ilivyo,” amesema Bw Okeyo.

Mkurugenzi wa chuo kilichofungwa cha Matric Institute Bw Samuel Kachumbi amesema atafuata maagizo yote aliyopewa lakini atapata hasara kubwa kutokana na masharti hayo.

“Kutokana na yale yaliyotendeka nitahakikisha nimefuata maagizo yote. Hata ingawa wamevuruga mambo yetu, tutajikaza tuwezavyo,” amesema Bw Kachumbi.

You can share this post!

RAGA YA DUNIA U-20: Chipu yatafunwa na Uruguay kama njugu...

KILIMO: Mimea inyunyiziwe maji kwa wingi baada ya...

adminleo