Habari Mseto

Walimu, wazazi walia shule kuchafuliwa

July 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na IAN BRYON na PETER MBURU

WANAFUNZI na walimu wa shule ya msingi ya Rayudhi, Kaunti ya Migori walipigwa na mshtuko alhamisi, wakati walipofika shuleni na kupata ubao na kuta za darasa zikiwa, ashakum si matusi, zimepakwa mavi.

Walipowasili shuleni asubuhi, wanafunzi hao wa darasa la nane pamoja na walimu wao walishangaa baada ya kulemewa na harufu mbaya, na walipoingia darasani ndipo wakabaini kuwa ubao na kuta zilikuwa zimepakwa choo cha binadamu.

Tukio hilo lilishangaza jamii ya shule na majirani, kwani kando na ubao na kuta, sehemu za kuwashia stima pia zilikuwa zimechafuliwa.

Ni hali ambayo ilisambaratisha shughuli za masomo kwa saa kadhaa, baada ya wasimamizi wa shule kuwatuma wanafunzi nyumbani kuita wazazi, wajionee tukio hilo.

Hata hivyo, kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo Michael Agutu, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwao kushuhudia kisa cha aina hiyo, akisema kuwa kwa miaka mitatu iliyopita, wamekuwa wakishuhudia.

Aidha, mwalimu huyo alitaja kitendo hicho kuwa cha kishirikina na kilicholenga kuwasumbua watoto.

Kitabu chachafuliwa

Bw Agutu alisema kuwa wiki iliyopita, mwanafunzi alipata vitabu vyake vikiwa vimeraruliwa na kupakwa choo cha binadamu.

Mwalimu huyo alisema kuwa sasa walimu wameamua kutumia njia za maombi kuona ikiwa watasaidia hali, kwani watoto wameshtuka na kuathirika kisaikolojia.

“Wazazi sharti wahusike katika utafutaji suluhu kwa hili tatizo. Imewazidi watoto kuwa wakipata mavi darasani kila wakati,” akasema Bw Agutu.

Lakini wakati huu kinachoshangaza ni kwanini mhusika aliamua kulenga darasa la nane, ambalo linatarajiwa kufanya mtihani wa kitaifa baadaye mwaka huu.

Mwenyekiti wa wazazi shule hiyo Zachary Okuyo aliwataka viongozi wa kidini kuombea shule hiyo, akisema inahangaishwa sana.

“Hatuamini kuwa hili linafanyika kwa shule iliyoko eneo letu. Tunawaomba viongozi wa kidini kuingilia kati kwani watoto wetu wameathirika kisaikolojia,” akasema.