Habari Mseto

Mbunge kortini kwa ulaghai wa Sh10m

July 12th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Nyakach Joshua Aduma Owuor alishtakiwa Ijumaa kwa kula njama ya kuilaghai Kaunti ya Nairobi kwa kuidhinisha wakili Stephen Mburu ambaye kwa sasa ni marehemu, alipwe kitita cha Sh10 milioni mwaka 2011.

Bw Owuor aliyekanusha mashtaka mawili mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya ufisadi, Bw Lawrence Mugambi, aliachiliwa kwa dhamana ya Sh3 milioni.

Bw Mugambi alimwamuru mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji asimruhusu mwanasiasa huyu kusafiri nje ya Kenya kwa sababu alidai kortini hana pasipoti anayoweza kutumia ziarani.

Alishtakiwa kuwa, kati Juni 3 na 7 mwaka 2011, akishirikiana na watu wengine walikula njama ya kuilagai Kaunti ya Nairobi Sh10 milioni kwa kuidhinisha malipo hayo kwa wakili Stephen Mburu ambaye kampuni yake ya mawakili inaitwa Wachira, Mburu, Mwangi Advocates.

Pia alishtakiwa kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake.

Kiongozi wa mashtaka Bi Hellen Mutellah alisema kati ya Februari 17 na Juni 16, 2011 akiwa Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria katika NCC aliidhinisha wakili Mburu ambaye alifariki dunia mwaka 2018, alipwe Sh10 milioni.

Kesi kuunganishwa

Bi Mutellah aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo itaunganishwa na ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero na wenzake walioshtakiwa kwa ulaghai wa Sh68 milioni.

“Hii kesi itaunganishwa na nyingine ambapo Dkt Kidero na washukiwa wengine 15. Naomba hii mahakama imwachilie mshtakiwa kwa kiwango cha dhamana ambayo Dkt Kidero na wengine waliachiliwa cha Sh8 milioni pesa tasilimu,” alisema Bi Mutellah.

Pia aliomba mshtakiwa aagizwe awasilishe pasipoti yake kortini na asitembelee afisi za kaunti wala kuzugumza na mashahidi.

Lakini wakili Fred Okeyo alipinga ombi hilo na kueleza korti, “Mshtakiwa hajawahi kufanya kazi na kaunti ya Nairobi. Alikuwa ameajiriwa na lililokuwa baraza la jiji la Nairobi kabla ya mfumo wa ugatuzi kuanzishwa 2013.”

Korti iliorodhesha kesi itajwe Julai 19.

Punde tu baada ya kupewa dhamana hiyo ya Sh3 milioni, wakili wake aliomba korti iipunguze akisema hawezi kupata dhamana hiyo lakini hakimu akakataa kuibatilisha.”