• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:55 AM
FUNGUKA: ‘Kazi ya dume ni kumaliza uchu tu’

FUNGUKA: ‘Kazi ya dume ni kumaliza uchu tu’

Na PAULINE ONGAJI

WAREMBO wengi wanapoulizwa mipango yao ya siku za usoni, mbali na kujiimarisha kitaaluma, baadhi yao watakuambia ni nkuolewa na kuwa na familia zao.

Hayo sio maazimio ya Annette, Elin, Winnie na Melisa, kikundi cha warembo wanne ambao kwa baadhi ya watu, urafiki wao sio wa kawaida.

Japo ndoto zao kwa upande wa taaluma zimetimika, hawana haja ya kuzitimiza katika masuala hayo mengine niliyotaja awali. Hebu kwanza nikutambulishe kwa mabinti hawa.

Annette ana umri wa miaka 34 na ni mfanyabiashara maarufu jijini Nairobi ambapo anamiliki vilabu kadha na fleti kibao.

Hii inamaanisha kwamba katika masuala ya kifedha, anamudu kumshughulikia bintiye bila hofu ya kulemewa.

Winnie, 35, kwa upande wake ni daktari wa watoto katika mojawapo ya hospitali zinazofahamika nchini.

Ni suala ambalo limemhakikishia mshahara mzuri na hivyo kumwezesha kuwekeza katika biashara tofauti. Ni mama wa watoto wawili.

Elin naye ana umri wa miaka 36 na ni mkuu wa idara ya ukaguzi wa mahesabu katika shirika moja la kimataifa ambalo lina tawi lake hapa nchini.

Pia yeye mshahara wake ni wa juu, suala linalomwezesha kukidhi mahitaji yake na ya wanawe watatu bila wasiwasi.

Kwa upande mwingine Melisa, 39, ni meneja katika shirika moja lisilo la kiserikali.

Kwa zaidi ya miaka 15 ambayo ameajiriwa pale, amefanya kazi na mashirika mbalimbali kama mtaalamu wa kifedha hivyo kumwezesha kuwekeza na kujitegemea kifedha.

Marafiki wa karibu

Wanne hawa ni marafiki wa karibu, uhusiano ulioanza wakiwa bado makinda.

Wote tumetalikiana na waume zao kutokana na sababu tofauti. Na kutokana na masaibu ambayo wote wameshuhudia katika mahusiano, hawana haja na wanaume.

Mmoja wao anazumgumza kwa niaba ya hawa wengine:

“Badala yake tumeamua kuwekeza katika uhusiano wetu kama marafiki wa dhati. Kwa hivyo kwa zaidi ya miaka kumi tumekuwa tukikutana angaa mara mbili kwa mwezi kubarizi kwa kuhudhuria tamasha mbalimbali na kuzuru maeneo tofauti.

Tukiwa klabuni huwa tunaketi pamoja na kaka fulani akivutiwa na mmoja wetu, basi sisi humualika kwenye meza yetu na hata kumnunulia kileo na akishatosheka hana budi kushika hamsini zake.

Sote tunajitegemea kifedha na hivyo hatuna haja na mwanamume. Kila tunapokumbwa na uchu wa mahaba, kila mmoja ana uhuru wa kumtafuta kaka wa kumsaidia kuzima kiu yake ya wakati huo.

Hatutaki kuolewa tena. Badala yake, tumewekeza katika shamba tulilonunua ambapo tayari tushajenga jumba kubwa huku tukitarajia kuishi sote pamoja pindi tutakapostaafu.

Katika hesabu zetu, hakuna nafasi ya mwanamume, pengine tu wa kumaliza uchu.

Ushauri wetu kwa wasichana ni kujipenda, kujikubali na kukumbatia urafiki kama wetu badala ya kupoteza muda wao wakiolewa na wanaume wasiowaongezea chochote maishani mwao.”

You can share this post!

NGUGI: Ukweli ni kwamba Wakenya walia; mzigo haubebeki

CHOCHEO: Kutafsiri ndoto za mapenzi

adminleo