Wa Iria awafaa wakulima wa Kakamega kwa kuwapiga jeki ya miche 10,000 ya miparachichi
Na SHABAN MAKOKHA
WAKULIMA katika Kaunti ya Kakamega ambao wamekuwa wakitegemea sana ukuzaji wa miwa sasa wametakiwa kuzingatia kilimo cha parachichi kama njia mojawapo ya kubadilisha mtazamo na vilevile kuimarisha njia za kujipa kipato.
Gavana wa Kaunti ya Murang’a, Bw Mwangi Wa Iria alisema Ijumaa kwamba kampeni ya hamasisho kwa wakulima kuzimngatia uzalishaji wa parachichi imeshika kasi nchini Kenya na wakulima wa Kakamega hawafai kuachwa nyuma.
Alisema hayo mara baada ya hafla chini ya Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambapo vijana na wanawake walifuzu katika mpango wa Kaunti ya Kakamega wa Huduma ya Vijana na Kuwainua Kima Mama.
Wa Iria aliwapa wakulima miche 10,000 ya miparachichi kama sehemu ya kuwapiga jeki kukumbatia kilimo hicho.
Shughuli hiyo ilifanyika katika uwanja wa Bukuhungu.
“Nimekuja huku na bila shaka nawaachia zawadi nzuri ambayo ni miche 10,000 ya miparachichi ambayo naona itakuwa kilimo mbadala kwa kile cha miwa ambacho matokeo yake yamekuwa ni hasara kwa wakulima,” alisema Wa Iria.
Aliongeza kwamba aina ya Hass hustahimili hali kadhaa za hewa na kwamba huchukua miaka mitatu kuanza kuzaa matunda.
Mparachichi mmoja una uwezo wa kuzaa kwa mwaka mfululizo na unaweza kuzaa hadi kilo 100 za matunda.
Nchini Kenya, maparachichi huzalishwa kwa wingi Murang’a, Nyeri, Kirinyaga, Embu na Meru, lakini imeanza kupata umaarufu Kakamega, Vihiga, Bomet, Kericho, Kisii na Nyamira.
Gavana Oparanya naye alisikitika kuyumbayumba kwa Kampuni ya Sukari ya Mumias kumechangia kuzorota kwa hali ya uchumi Kakamega.
“Eneo hili linapitia hali ngumu kwa kutegemea tu kilimo cha mahindi na miwa,” alisema Gavana Oparanya.