• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Kilimo: Ukuzaji wa mimea inayozaa kwa muda mfupi umemfaidi pakubwa

Kilimo: Ukuzaji wa mimea inayozaa kwa muda mfupi umemfaidi pakubwa

Na SAMMY WAWERU

BI Judith Nduva ambaye ni mfanyakazi katika Wizara ya Fedha anasema ilikuwa vigumu kufanya maendeleo na kujiimarisha kimaisha kwa kutegemea pahala pamoja tu.

Hata hivyo, alipokata kauli kuwekeza katika shughuli za kilimo, mambo yalibadilika.

“Nimepiga hatua nyingi na kubwa kimaendeleo, na kamwe sijutii kufanya ukulima,” anasema Bi Nduya, mama wa watoto watano.

Safari iling’oa nanga 2013 kwa mtaji wa Sh200,000 alizokuwa ameweka kama akiba.

Bi Nduva anasema alikodi ekari nne eneo la Loitoktok na kukuza vitunguu saumu.

Anaeleza kwamba msimu wa kwanza hakupata faida yoyote, ila mavuno aliyopata yalimrejeshea mtaji pekee. Vitunguu saumu huvunwa miezi minne baada ya upanzi.

Kulingana na mama huyu ni kwamba licha ya pigo hilo hakufa moyo, na msimu wa pili na wa tatu alianza kuonja matunda ya juhudi zake.

“Kila msimu ulinipa faida ya Sh100,000,” adokeza.

Changamoto kuu ilikuwa kiini cha maji.

Ili kutatua hilo, alihamia eneo la Korrompoi, karibu kilomita 15 kutoka mtaa wa Kitengela na kukodi ekari nne pia.

Humo anasema alichimba shimo la maji lenye urefu wa futi 150 na kuwekeza kwa vitekamaji au vihifadhi maji. Pia alinunua mifereji ili kukumbatia mfumo wa kisasa kunyunyizia maji mashamba kwa mifereji (Irrigation).

Hatua hiyo ilimgharimu zaidi ya Sh200, 000.

Ukizuru mradi wake maarufu kama Kituasi Orchad, kinachokulaki ni rangi ya kijani. Anakuza mboga asili, yaani zile za kienyeji kama mnavu, kunde, mchicha, saga na mrenda.

Pia, mkulima huyu ni mzalishaji wa giligilani maarufu kama dania, spinachi na sukuma wiki. Kadhalika anasema hajaasi ukuzaji wa vitunguu saumu, ambapo pia amejumuisha vile vyekundu vya mviringo.

Judith anasema sababu hasa zilizomchochea kupanua mawazo na kuanza kukuza mboga aina mbalimbali haswa zile asili na dania zinatokana na gharama yake ya chini katika kupanda, kutunza bila kusahau ni mazao yenye mapato ya haraka.

“Mboga za kienyeji ni mithili ya mahamri moto sokoni. Hupandwa kwa mfumo asili, kilimohai, ambapo ni vigumu kuathirika na wadudu na magonjwa ya mimea. Hivyo basi ni nadra kupuliziwa dawa,” anafafanua.

Kilimohai ni mfumo wa zaraa unaotumia mbolea ya mifugo au ndege kama vile kuku, ambayo pia inaweza kuchanganywa na matawi na majani. Mbolea hiyo maarufu kama mboji au vunde, hupewa muda iive sawaswa.

Isitoshe, kilimo cha aina hii hakitumii kemikali, kwani ni vigumu mimea na mazao kushambuliwa na wadudu na magonjwa.

Judith Nduva anaendelea kueleza kuwa kilichomshinikiza zaidi kukuza mboga za kienyeji ni kuwa huchukua muda mfupi kuanza kuvunwa baada ya upanzi, kando na gharama ya upanzi na utunzaji kuwa nafuu.

“Mboga asilia huanza kuvunwa mwezi mmoja baada ya upanzi. Mnavu na mchicha huendelea kuvuna kwa kipindi au muda wa miezi miwili ama mitatu mfululizo. Cha muhimu ni maji na palizi dhidi ya makwekwe,” aeleza. Giligilani-dania, huanza kuvunwa kuanzia siku ya 45 baada ya upanzi.

Bw James Murage, mtaalamu wa kilimo anahamasisha wakulima mbali na kukuza mimea inayochukua muda mrefu kuzalisha, haja ipo wapande inayozalisha kwa muda mfupi.

Akitoa mfano wa mboga za kienyeji, spinachi na sukuma wiki, mdau huyu anasema kilimo chake kikitiliwa maanani kitainua kimapato na kimaendeleo anayekizamia.

“Idadi kubwa ya Wakenya hutumia mboga na hii ina maana kuwa soko lake halitakosa. Wanaozikuza haswa za kienyeji, ni kitega uchumi cha haraka,” anasema Bw Murage.

Idhinisho

Hata hivyo, anahimiza umuhimu wa kuzingatia taratibu za kitaalamu zinazojumuisha pembejeo; mbolea, mbegu na dawa.

“Kuna pembejeo nyingi bandia sokoni hasa mbegu. Mkulima asipokuwa makini, hilo linaweza kuwa kikwazo dhidi ya kuhitimu lengo la mazao bora,” anaonya, akishauri kutumia pembejeo zilizoidhinishwa na taasisi husika za serikali.

Bw Murage, ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya mbegu kutoka kampuni ya Safari Seeds anahimiza wakulima kupiga msasa kampuni kwa kuzingatia historia yao, ikiwa ni pamoja na ufanisi wa wakulima wanaotumia bidhaa zao.

Mtazamo wake unatiliwa maanani na Judith Nduva, akiungama kuwa amefanikisha safari yake katika kilimo kwa kuzingatia uhalisia wa pembejeo.

Mwanazaraa huyu anasema hatua ya kukumbatia mfumo wa kilimohai na kunyunyizia mashamba maji kwa mifereji pia imemuwezesha kuzalisha mazao kwa wingi, ikizingatiwa kuwa amewekeza pakubwa katika mimea inayozalisha kwa kipindi kifupi.

Aidha, amegawanya shamba lake lenye ukubwa wa ekari nne kwa makundi ya nusu ekari kwa kila mazao. “Huhakikisha kila mwezi sikosi mazao shambani ili kuafikia mahitaji ya wateja wangu,” asisitiza Bi Nduva. Wateja wake ni wa kijumla, ambao huendea mazao shambani.

You can share this post!

Cheruiyot ahifadhi taji lake Riadha za Diamond League

DAU LA MAISHA: Awika katika nyanja inayochukuliwa kuwa ni...

adminleo