Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia ya makutano na mwachano katika mahusiano baina ya wanajamii

July 13th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

Katika makala iliyotangulia, tuliangazia mada kuhusu nadharia ya utambulisho katika kufafanua michakato ya uteuzi wa lugha.

Hii leo tutapambanua kwa kina nadharia ya mwachano na makutano katika Kiswahili.

Kulingana na Kihore na wenzake, nadharia ya makutano na mwachano hujaribu kupima mshikamano uliopo miongoni mwa wanajamii lugha kuhusu utamaduni wao na lugha yao kama mbinu ya kupima nguvu ya utambulisho wa jamiilugha husika.

Nadharia hii inasisitiza kuwa ni kazi ya wanajamiilugha wenyewe kuhamasika na kukuza lugha yao na kuitumia ili iweze kuelezea amali za jamii lugha, mielekeo yao na makundi yao na jinsi ambavyo lugha yao ni tofauti na lugha nyingine.

Kwa upande mwingine, makutano huboresha mawasiliano kwa sababu hupunguza mashaka, dukuduku kati ya watu na kufanikisha maelewano.

John-Weiner (1998) (akinukuliwa na Wardhaugh) anatumia nadharia ya utambulisho kuelezea namna mbalimbali za uteuzi wa lugha.

Mwanaisimu huyu anaeleza namna jamii lugha moja inaweza kuamua kutumia lugha ama kujihusisha na jamiilugha nyingine (makutano) au ikatumia lugha kujitenga na jamii lugha nyingine (mwachano).

Naye Keller (1989), anaeleza kwamba utambulisho wa mtu umefungamana na mambo mengine mathalani:

i. lugha

ii. utamaduni

iii. historia ya jami

iv. siasa

v. uchumi

vi. dini

vii. vyakula na kadhalika

Jambo linalojitokeza bayana ni kwamba, kipengele kimoja au viwili havitoshi kubainisha utambulisho wa mtu, jamii au taifa.

Kimsingi utambulisho wa mtu umejikita ndani ya utamaduni wa jamii lugha ambamo mzungumzaji anayetakiwa kubainisha utambulisho wake ni sehemu yake.

Sifa bainifu za mzungumzaji

Tabouret Keller, anafafanua dhana ya utambulisho kwa kutaja sifa tatu bainifu za kimsingi ambazo zinapaswa kuzingwatiwa katika kumtambulisha mzungumzaji. Sifa au vipengele hivyo ni pamoja na:

i. Kigezo cha lugha ya mzungumzaji ambapo anauita utambulisho wa nje unaosikika.

ii. Kigezo cha mahali alikozaliwa mzungumzaji ambako lugha anayotumia ndiyo lugha kuu ya mawasiliano.

iii. Mzungumzaji anapaswa kujiona kuwa sehemu ya jamii lugha na kuwa ataendelea kuitumia lugha yake ili kuidumisha.

 

[email protected]

Marejeo

Ogechi, N.O. (2002). Mbinu za Mawasiliano Kwa Kiswahili. Eldoret: Moi University Press.

Pride, J.B. (1971). The social meaning of language. London: Oxford University Press.

TUKI (2000). Swahili – English Dictionary . Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (kwa sasa ikifahamika TATAKI).