Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya tamathali za usemi katika mawasiliano

July 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

KWA mujibu wa Ogechi (2002:12), tunawasiliana ili kuwaathiri wengine.

Kwa mfano, matumizi ya vibonzo katika magazeti huwa ni ya kufanikisha mawasiliano, ijapokuwa wengi huwa wanapuuza kuzingatia kwa makini jumbe zinazokuwa pale ndani, aghalabu yaweza kuthibitishwa, kufasiliwa na kubainishwa kwa kutumia data.

Kwa mfano, vibonzo hutumiwa katika magazeti ili kufanya suala nyeti au changamano kuonekana rahisi kwa njia ya ucheshi na swala hilo kuonekana silo la tatizo mno; au ukipenda kupunguza makali ya maneno.

Jamii fulani huenda imebanwa na janga fulani lakini wasanii wanaweza kutumia vibonzo kwa ubunifu kwa njia itakayorahisisha hali hiyo.

Mawasiliano kwa njia ya maandishi kama vile yana manufaa mbalimbali kama zifuatazo:

i. Ujumbe unaweza kudurusiwa mara kadhaa kabla ya kuusambaza na kuhifadhiwa.

ii. Vilevile ujumbe hubaki kuwa ule ule hata baada ya muda mrefu.

iii. Hutumiwa kuwasilisha mawazo nyeti au changamano

iv. Mawasiliano kwa njia ya maandishi yanaweza kudhibitiwa, kufasiliwa, na kubainisha mawasiliano.

Dhana ya tamathali za usemi katika mawasiliano

Kwa mujibu wa Wamitila (2003), tamathali ni neno au kifungu ambacho kina maana iliyofichwa.

Tamathali ni mojawapo ya mbinu za matumizi ya lugha ya mkato na ya kisanii.

Tamathali za lugha humwezesha mtunzi kusema mengi kwa maneno machache yenye mvuto, mguso, na mnato.

Mbinu au fani za lugha 

Huu ni uteuzi wa maneno ili kuifanya lugha iwe ya kupendeza na kuvutia. Pia hujulikana kama Mapambo ya Lugha. Fani za Lugha zinaweza kutambulikana moja kwa moja bila kusoma kifungu kizima.

Mbinu za sanaa

Ni ubunifu wa kisanaa unaojitokeza baada ya kusoma au kusikiliza masimulizi.

Angalau unahitaji kusoma sentensi kadhaa au hata hadithi nzima ili kutambua mbinu ya sanaa iliyotumika.

Kuna tamathali mbalimbali za usemi jinsi tutakavyozijadili ifuatavyo:

Sitiari (Imagery)

Kwa mujibu wa Mbatia (2000), anaeleza sitiari kama ulinganishi usio wa moja kwa moja kwani hautumii viunganishi vya ulinganishi kama vile, mithili ya, ja, au kama.

Naye Msokile (1993), anasema kuwa sitiari ni tamathali ya usemi inayolinganisha au kuhusisha vitu vilivyo tofauti kwa kitabia au kimaumbile.

Aidha, Msokile anaendelea kusema kuwa vitu au viumbe viwili vilivyo tofauti kitabia au kimaumbile iliyopo kati ya vyote viwili ama zaidi bila ya kutaja dhahiri sifa hiyo. Dhana ya sitiari hivyo basi inahusisha ulinganishi wa vitu viwili na kuvifanya vionekane kama vyenye sifa za kufanana ilhali vitu hivi ni tofauti kabisa.

[email protected]

Marejeo

Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania.” Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

Mtembezi, I. J. (1997). “Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia”. Dar es Salaam.