• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Mbunge sasa aunga maoni ya Muthaura

Mbunge sasa aunga maoni ya Muthaura

Na CHARLES WANYORO

MBUNGE wa Imenti Kaskazini Rahim Dawood, ameunga mkono pendekezo la aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Francis Muthaura kwamba Katiba ifanyiwe marekebisho kuruhusu mshindi katika uchaguzi wa urais kubuni serikali ya muungano na anayeibuka wa pili.

Bw Dawood pia aliunga mkono wazo la kuongezwa kwa idadi ya nyadhifa za juu serikalini ili kushirikisha watu wengi.

Akihutubia waombolezaji wakati wa mazishi ya Bw Titus Mburugu ambaye hadi kifo chake alikuwa Naibu Kamishna wa Kaunti, mbunge huyo alisema hiyo ndio njia ya pekee kuimarisha uwiano na utangamano nchini.

Bw Dawood alisema kubuniwa wadhifa wa Waziri Mkuu kutaongeza mzigo wa mishahara ya watumishi wa umma kwa kiwango kidogo zaidi hali ambayo alisema itarekebishwa kupitia kuimasharishwa kwa vita dhidi ya ufisadi.

Akitoa mapendekezo yake kwa Kamati ya Maridhiano (BBI), Bw Muthaura alipendekeza kuwa anayeibuka wa pili katika uchaguzi wa urais ateuliwe kuwa Waziri Mkuu lakini Rais aendelee kuwa kiongozi wa serikali na taifa.

Vilevile, Bw Muthaura alipendekeza kuwa wadhifa wa Naibu Rais uendelee kuwepo.

Wakati huo huo, Bw Dawood amepinga pendekezo la chama cha Thirdway Alliance, kupitia mpango wake wa Punguza Mzigo, kwamba idadi ya wabunge na madiwani ipunguzwe, akisema hatua hiyo itaokoa Sh10 bilioni pekee ilhali zaidi Sh600 bilioni hupotea kupitia kwa ufisadi.

“Punguza Mzigo ni wazo zuri lakini si suluhisho kwa gharama ya juu serikalini. Tunafaa kulenga mabilioni ya fedha yanayopotea kupitia ufisadi. Ukipunguza idadi ya nafasi za uwakilishi utapunguza kiasi cha fedha kisichozidi Sh10 bilioni. Tulenge Sh600 bilioni zinazopotea kupitia ufisadi,” aliwaambia waombolezaji.

Pingamizi

Kwa mara ya kwanza, Bw Dawood alikiri kuwa alihudhuria mkutano katika mkahawa wa La Mada kujadili ajenda ya maendeleo katika eneo la Mlima Kenya.

Mkutano huo uliibua pingamizi kutoka kwa wanasiasa fulani baada ya madai kuibuka kwamba ulijadili njama ya mauaji ya Naibu Rais William Ruto.

Alisema wale wanaohusisha jina la Waziri wa Biashara Peter Munya katika njama hizo wana nia chafu ya kuzima nyota yake ya kisiasa.

“Wabunge wengi kutoka kaunti 10 za Mlima Kenya huhudhuria mikutano ya maendeleo katika maeneo ya Nyeri, Naivasha na mhakawa wa La Mada. Hatujawahi kujadili Dkt Ruto kwa sababu wafuasi wake pia huhudhuria. Si hatia kwa viongozi kutoka Mlima Kenya kukutana kwa ajili ya maendeleo,” akasema Dawood.

Vile vile, alimtaka Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jina (DCI) George Kinoti kukagua kanda ya Bw Denis Itumbi aliyodai inasheheni ushahidi kuhusu njama ya muaji ya Naibu Rais.

You can share this post!

Benki zasema kuna uhaba wa noti mpya nchini Kenya

KINAYA: Wabunge wajilipe vinono, nasi pia watulipe kabla ya...

adminleo