Makala

MWANASIASA NGANGARI: Mwanasheria Mkuu aliyekuwa na ushawishi kwa Kenyatta, Moi

July 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na KENYA YEAR BOOK

CHARLES Mugane Njonjo anakumbukwa kama Mwanasheria Mkuu ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa kwenye serikali ya Mzee Jomo Kenyatta.

Alizaliwa mnamo Januari, 23, 1920 katika eneo la Kabete, Kaunti ya Kiambu, kwenye familia ya watoto wanane; wavulana wanne na wasichana wanne. Ni mwanawe Bw Josiah Njonjo, ambaye alihudumu kama chifu katika serikali ya kikoloni. Dada zake watatu wangali hai.

Na licha ya wakosoaji wake kumtaja kama anayechukia kila kitu chenye asili ya Kiafrika, amekuwa akipinga dhana hiyo. Hilo ndilo lilowafanya baadhi ya wandani wake serikalini kumpa jina ‘The Duke of Kabeteshire’ kwa uraibu wa mienendo na mavazi ya Kizungu.

“Miye na binamu yangu tulikuwa tukitumia muda mwingi katika makazi ya nyanyangu, ambapo alikuwa akitutambia ngano. Alitupa chakula asili cha Kiafrika. Alinipenda kwa kuwa nilipewa jina la mumewe,” asema.

Utotoni mwake, Njonjo hakuwa na marafiki wengi, ikizingatiwa kwamba babake alikuwa chifu. Ilimlazimu kucheza na mabinamu wake.

Alianza masomo yake katika Shule ya Msingi ya Gwa Giteru katika eneo la Lower Kabete.

Shule hiyo iliitwa hivyo kwani ilihusishwa na Canon Leakey, ambaye ni babuye mwanasiasa Richard Leakey.

Alijiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance, ambako alisoma pamoja na watu maarufu kama Jeremiah Nyaga. Bw Nyaga alikuwa miongoni mwa watu walioteuliwa na Mzee Jomo Kenyatta kuhudumu katika baraza la kwanza la mawaziri.

Njonjo anasema kuwa maisha katika shule hiyo hayakuwa rahisi.

“Hatukuruhusiwa kuvaa viatu. Tulikuwa pia tukioga kwa maji baridi. Ni katika shule hii ambako nilikula ugali kwa mara ya kwanza,” anakumbuka.

Mnamo 1939, alijiunga na Taasisi ya King’s, Budo nchini Uganda, ambako alisoma kwa miaka miwili kabla ya kujiunga na chuo kikuu. Alikuwa katika darasa moja na Frederick Mutesa, ambaye baadaye alichaguliwa kama Kabaka (mfalme) wa Wabaganda. Baada ya hapo, babake alimtaka kwenda Uingereza kwa masomo lakini mpango huo haukufaulu. Badala yake, alienda katika Chuo Kikuu cha Fort Hare, nchini Afrika Kusini.

Ingawa alisomea taaluma ya sheria, masuala mengine aliyosomea ni utawala, soshiolojia na lugha ya Kilatino, aliyosema ilimsaidia sana alipomaliza kusomea shahada yake ya sheria.

Kulingana naye, maisha nchini Afrika Kusini yalikuwa magumu kutokana na mfumo wa utawala wa ubaguzi wa rangi.

“Ningesafiri kutoka Durban hadi Fort Hare, ambapo gari la moshi lilikuwa limegawanywa katika mabewa ya watu weusi na watu weupe,” asema.

Anaeleza kuwa katika nyakati zingine, walilazimika kubeba chakula chao, kwani hawangeruhusiwa kula katika maeneo ya Wazungu.

Alisoma katika chuo hicho kwa miaka mitatu. Baadaye, alirudi nchini kwa mwezi mmoja, ambapo alielekea katika Chuo Kikuu cha Exeter, nchini Uingereza kusomea diploma katika masuala ya utawala wa umma.

Njonjo alimaliza masomo yake katika chuo hicho mnamo 1947. Vilevile, alisomea Chuo cha Masuala ya Uchumi cha London hadi 1950. Alisomea sheria kwa miaka minne kabla ya kutawazwa rasmi kuwa wakili. Asema kuwa alikaa sana nchini Uingereza kwani alilazimika kufanya kazi za vibarua kugharamia maisha yake.

Alirejea Kenya mnamo 1954. Serikali ya kikoloni ilimwajiri kama msajili wa Mahakama Kuu ambapo alitumwa kuhudumu Pwani. Baadaye, alipandishwa ngazi. Alihamishiwa katika afisi ya Mwanasheria Mkuu kama mojawapo ya wasimamizi wake wakuu.

Mwaka mmoja kabla ya uhuru, alipandishwa ngazi tena na kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma. Hiyo ilikuwa hatua chache tu kabla ya kutangazwa kuwa Mwanasheria Mkuu.

“Wakati Mzee (Jomo Kenyatta) alitangazwa Waziri Mkuu, niliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu. Wakati Kenya ilijinyakulia uhuru wake mnamo 1964, niliteuliwa kama mmoja wa wabunge na mshiriki wa Baraza la Mawaziri,” asema.

Bw Njonjo alikuwa miongoni mwa viongozi wachache ambao waliaminiwa sana na Mzee Kenyatta. Nyakati nyingi, alikuwa akisafiria katika gari la kibinafsi la Mzee Kenyatta, ambaye pia alitafuta ushauri wake kabla kufanya baadhi ya maamuzi muhimu.

Ukaribu wa wawili hao ulikuwa mkubwa kiasi kwamba, inaaminika kuwa Njonjo ndiye alimshauri Mzee Kenyatta kumteua Rais Mstaafu Daniel Moi kama makamu wake wa rais wa tatu, baada ya Bw Joseph Murumbi kujiuzulu. Inaelezwa kuwa Mzee Kenyatta hata alimshukuru Njonjo kwa ushauri wake kuhusu uteuzi wa Mzee Moi.

Majukumu

Kama Mwanasheria Mkuu, Bw Njonjo alisimamia mashtaka ya umma, kesi zilizoikabili serikali, uchunguzi wa mashtaka ya jinai na uandaaji wa sheria. Changamoto kuu iliyomkumba awali ni kubadilisha sheria kandamizi za kikoloni, hasa zile ziliozowazuia Waafrika kununua mashamba katika baadhi ya maeneo nchini. Sheria hizo pia ziliwazuia kwenda hospitali na shule sawa na Wazungu.

Akiwa Mwanasheria Mkuu, katiba ilifanyiwa mageuzi mengi. Hata hivyo, mageuzi hayo yalilenga kuongeza mamlaka ya rais maradufu. Katika kutekeleza mageuzi hayo, Njonjo alikumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa Bunge, hasa kutoka kwa kundi la wabunge saba vijana aliloiita “Dada Saba Wenye Ndevu” (The Seven Bearded Sisters). Wanasiasa hao ni Koigi wa Wamwere, Mwashengu wa Mwachofi, James Orengo, marehemu Chelegat Mutai, Abuya Abuya, Onyango Midika na Lawrence Sifuna.

Asema kuhusu kundi hilo: “Wakati mwingine Bunge lilikuwa la kufurahisha. Kundi hilo la wabunge lilikuwa likijaribu kutumia werevu wake kuzima ajenda za serikali lakini wakashindwa.”

Bw Njonjo pia atakumbukwa kwa kuendesha mageuzi ya haraka ya katiba kupitia Bunge ili kumruhusu Mzee Kenyatta kumsamehe mwanasiasa Paul Ngei, baada ya mahakama kumzuia kuwania ubunge kwa kukiuka sheria za uchaguzi. Vilevile analaumiwa kwa kuruhusu baadhi ya wabunge wenzake kushtakiwa licha ya rai za msamaha kwa Mzee Kenyatta.

Njonjo alioa mnamo Novemba 20, 1972 akiwa na umri wa miaka 52. Asema alioa akiwa amechelewa kutokana na “majukumu mengi yake ya kikazi.” Asema kuwa katika baadhi ya nyakati, alilazimika kuahirisha kikao na mpenziwe kutokana na kazi.

Mnamo 1976, kundi la wanasiasa kutoka maeneo ya Kati, Bonde la Ufa na Mashariki walianza kundi lililoitwa ‘Change-the-Constitution Movement’ ambalo lengo lake kuu lilikuwa ni kubadilisha katiba, ili kuhakikisha kuwa Bw Moi hakuchukua uongozi kama Kaimu Rais ikiwa Mzee Kenyatta angefariki.

Hata hivyo, Njonjo alipinga juhudi zao, akizingatia Katiba kwa kumuunga mkono Bw Moi.

Alilikabili vikali kundi hilo, akisisitizia kuwa ni ‘makosa kufikiria kuhusu kifo cha rais.’

Baadhi ya wanasiasa walioendesha juhudi hizo ni Njenga Karume, Kihika Kimani, Paul Ngei na Jackson Angaine.

Njonjo alijiuzulu kama Mwanasheria Mkuu mnamo 1980, baada ya kuhudumu tangu 1963. Aliwania ubunge katika eneo la Kikuyu na kuchaguliwa. Aliteuliwa kuwa Waziri wa Haki na Masuala ya Katiba hadi 1983, alipofunguliwa mashtaka ya kujaribu kuipindua serikali ya Moi. Bw Moi alimteua Jaji Cecil Miller kumchunguza.

Hata hivyo, Njonjo huwa anasisitiza kwamba hakuwa na lengo la kuipindua serikali.

Akiwa na umri wa miaka 99, Njonjo angali mchangamfu na huchangia mara kwa mara katika masuala ya kitaifa. Amewekeza katika biashara nyingi.

Alihudumu kama mwenyekiti wa Benki ya Stanbic, hadi alipojiuzulu majuzi.