MAHINDI: Fyata ulimi, Kiunjuri amwambia Raila
GRACE GITAU, DENNIS LUBANGA na BARNABAS BII
WAZIRI wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri amempuuzilia mbali Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga kuhusu suala la uagizaji mahindi kutoka mataifa ya kigeni na kumtaka akome kuingilia masuala yanayohusu kilimo cha mahindi.
Wiki iliyopita, Bw Odinga alisema amefanya mikutano na wadau mbalimbali wakiwemo wakulima na idara inayosimamia hifadhi ya nafaka ya dharura, akabainisha hakuna uhaba wa mahindi inavyodaiwa na Wizara ya Kilimo.
Lakini Jumapili, Bw Kiunjuri alisema uhaba wa mahindi upo na akamkashifu Bw Odinga pamoja na viongozi wengine wanaokana uhaba huo. Kulingana naye, viongozi aina hiyo wanaingiza siasa katika suala hilo ilhali uagizaji mahindi kutoka nje si uamuzi wake bali ulikuwa uamuzi wa baraza la mawaziri.
“Uagizaji mahindi ya ziada utasaidia kusawazisha bei ya unga wa mahindi ambayo imekuwa ikipanda. Hatuna mahindi ya kutosha katika nchi hii na inatarajiwa bei ya unga itazidi kuongezeka. Kama uko katika biashara ya kuuza dhahabu, achana na mjadala kuhusu mahindi,” akasema Bw Kiunjuri.
Alisema hayo huku viongozi kutoka maeneo yanayokuza mahindi kwa wingi sasa wakipanga kwenda kortini kupinga mpango huo wa kuagiza mahindi kutoka nje, na kuyaingiza nchini bila ushuru.
Viongozi hao wamesema kuwa hatua hiyo itatoa nafasi kwa wahuni ndani ya serikali kuendelea kuwanyanyasa wakulima, hasa wakati huu ambapo imesalia miezi mitatu kwa wakulima kuanza kuvuna zao hilo.
Wakiongozwa na Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula na wabunge kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa , viongozi hao walisema mpango wa wizara ya Kilimo kuagiza mahindi kutoka nje haufai.
“Kama viongozi kutoka maeneo kunakokuzwa mahindi, hatuna jambo lingine la kufanya ila kuhamasisha wenzetu Seneti na Bunge la Kitaifa kwenda kortini kuzuia jaribio la Wizara ya Kilimo kuwanyanyasa wakulima, kwa kuingiza mahindi bila kuyatoza ushuru, wakati msimu wa mavuno unaelekea,” Bw Wetang’ula akasema.
Viongozi hao pia wamemtaka Bw Kiunjuri kujiuzulu, wakimlaumu kuwa ameshindwa kutekeleza majukumu ya wizara hiyo.
Kulingana na viongozi hao, kuna maafisa fulani wa serikali ambao tayari wana mahindi mengi nchi za nje, wanaosubiri kupewa mwanya huo kuyaleta na kufaidika wakati wakulima wanaumia.