Makala

OBARA: Mbona serikali inawaruhusu mabroka wa mahindi kuumiza wakulima?

July 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

KILA mwaka, Wakenya hukabiliwa na hali ngumu ya maisha wakati bei ya unga wa mahindi inapopanda.

Hivi sasa bei ya mfuko wa unga wa mahindi kilo mbili imepanda hadi Sh130 na inatarajiwa kuongezeka zaidi.

Chanzo cha hali hii ni madai kwamba kuna uhaba wa mahindi nchini, unaofanya bei ya nafaka hiyo kupanda na hivyo wasagaji unga kuongeza bei ya bidhaa zao.

Licha ya wasagaji unga kulalamikia uhaba wa mahindi, kuna baadhi ya wakulima wa zao hilo wanaosisitiza kuna nafaka za kutosha humu nchini ila bei ambayo serikali inataka kununua kupitia kwa Bodi ya Kitaifa ya Mazao na Nafaka (NCPB) ndio duni.

Wakati huo huo, kitengo cha kuhifadhi vyakula vinavyotumiwa wakati wa dharura pia kinasisitiza kungali kuna mahindi ya kutosha nchini, lakini kuna maafisa wa serikali wanaoungana na wasagaji unga kutetea uagizaji mahindi kutoka nchi za kigeni wakidai kuna uhaba.

Misimamo hii inayotofautiana kutoka kwa wadau wa sekta ya mahindi ni dhihirisho kwamba kuna watu wanachezea shere Wakenya.

Bidhaa muhimu kama vile mahindi, sukari na mafuta zimekuwa zikiingiziwa siasa kwa muda mrefu kwa manufaa ya watu wachache huku raia wa kawaida akitatizika kwa mzigo mzito wa gharama kubwa ya maisha.

Hii tabia ya mabwanyenye kushirikiana na maafisa wa serikali kubuni uhaba bandia wa bidhaa hizi muhimu ili wafaidike kwa kuziagiza kwa bei ya chini kutoka nchi za kigeni, inafaa kukomeshwa mara moja.

Lengo moja kuu la kuwepo NCPB ilikuwa ni kuepusha wakulima wa mahindi kulaghaiwa na madalali ambao hununua nafaka hizo kwa bei ya chini kisha kwenda kuuzia shirika hilo kwa bei ya juu.

Lakini inavyoonekana, NCPB imeshindwa kutekeleza jukumu hilo lake ipasavyo kwani sasa kuna madalali walionunua mahindi ya wakulima kwa bei ya juu kuliko ile iliyokuwa ikitolewa na serikali.

Tatizo limetokea kwamba, madalali hao wameishia kuficha nafaka walizonunua kutoka kwa wakulima ili kusubiri hadi wakati bei itakapopanda sokoni.

Hili ni dhihirisho wazi kwamba madalali wamezidi ujanja serikali, kwa hivyo itakuwa jambo la maana kwa serikali kutafakari upya jinsi ya kutafutia zogo hili suluhisho la kudumu.

Kuharakisha kuagiza mahindi kutoka nchi za kigeni mara kwa mara si suluhisho kama kweli kuna mahindi ya kutosha yaliyofichwa maghalani.

Ni vyema serikali itafute jinsi ya kukabiliana na mbinu hizi chafu za kibiashara za madalali na ipate ushirikiano mwema wa kibiashara na wakulima kwa njia itakayofaidi pande zote mbili.