• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Wakenya wapuuza kilio cha magavana

Wakenya wapuuza kilio cha magavana

LEONARD ONYANGO na VALENTINE OBARA

RAIA waliochoshwa na ulafi wa viongozi wa kisiasa nchini, wameonekana kutojali kilio cha magavana wanaodai serikali kuu inalenga kuangamiza ugatuzi kwa kuwanyima fedha.

Jana, magavana na maseneta walikusanyika Nairobi na kuandamana hadi Mahakama ya Juu kulalamika jinsi bajeti ya taifa ilivyopitishwa bila kupitisha mswada wa ugavi wa fedha kati ya serikali kuu na za kaunti.

Walitaka mahakama hiyo iamue kama hatua hiyo ilikuwa halali. Suala hilo litatajwa kortini Ijumaa.

Licha ya wakuu hao wa kaunti kulalamika mara kwa mara kwamba Bunge linatumiwa na serikali kuu kusambaratisha ugatuzi, hawajafanikiwa kushawishi wananchi kuwaunga mkono katika juhudi zao za kutaka fedha zaidi.

Wananchi mitaani waliendelea na shughuli zao za kawaida wakati magavana wakiandamana, huku wengine wakielekea kwenye mitandao ya kijamii kuwakejeli na kusema wamesababisha ‘ugatuzi wa ulafi’.

“Baraza la Magavana linasihi raia wote wajumuike kwenye wito huu wa kuokoa ugatuzi. Wakenya walichagua katiba mpya ili rasilimali ziwafikie karibu nao ili maisha yabadilike kupitia kwa huduma bora. Azimio hili linatishiwa na ni lazima tuinuke kulinda malengo ya katiba yetu,” akasema Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya.

Kupitia hashitegi ya #DevolvedGreed (uchoyo uliogatuliwa) kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Wakenya walisema idadi kubwa ya magavana hawajafanya maendeleo ya kuwanufaisha wananchi licha ya kupokea mabilioni ya fedha kutoka kwa serikali kuu.

“Ugatuzi umegeuka mzigo kwa walipa ushuru. Badala ya kuwanufaisha wananchi, magavana wanatumia fursa hiyo kupora hela za umma,” akasema Kevin Kinyua.

Magavana pamoja na madiwani hukashifiwa na wananchi kwa maisha yao ya kifahari yanayojumuisha safari za ng’ambo za mara kwa mara, na ununuzi wa magari ghali kupita kiasi mbali na jinsi wengine wao walivyonaswa kwenye sakata za ufisadi.

Maisha yao ya kistarehe yalizidi kushuhudiwa walipoandamana jijini Nairobi jana, kwani walilakiwa na wasakataji densi langoni mwa Mahakama ya Juu sawa na jinsi wageni waheshimiwa wanavyolakiwa wanapowasili katika viwanja vya ndege.

Bw Oparanya aliye pia Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, alisisitiza ugatuzi unaleta mafanikio na hakuna juhudi zozote za kuusambaratisha zitafanikiwa.

Mvutano kuhusu ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti umesababisha fedha zichelewe kutolewa kwa magavana, hali wanayosema inaathiri shughuli za kaunti.

Awali, Bunge la Kitaifa lilipendekeza Kaunti zipewe jumla ya Sh310 bilioni katika mwaka wa huu wa matumizi ya fedha 2019/2020 ulioanza Julai 1, ilhali Seneti ambayo imetwikwa jukumu la kupigania masilahi ya kaunti, ilipendekeza Sh335 bilioni.

Baada ya pande zote kushikilia msimamo makali, Naibu Rais William Ruto aliingilia kati ili kutafutia suala hilo ufumbuzi.

Dkt Ruto alifanya kikao kilichojumuisha magavana, wawakilishi wa Bunge la Kitaifa na Seneti, Mdhibiti wa Bajeti za Serikali na Tume ya Ugavi wa Mapato ya Serikali (CRA).

Bunge la Kitaifa lilikubali kuongeza mgao huo hadi Sh316 bilioni na Seneti ikalubali kupunguza kutoka Sh335 bilioni hadi Sh327 bilioni, ndipo mazungumzo yakakwama.

“Mazungumzo ya upatanishi yalisambaratika baada ya pande zote kushikilia msimamo mkali na ndiyo maana tumeamua kwenda mahakamani,” akasema Bw Oparanya.

You can share this post!

SIHA: Unywaji holela wa pombe unasababisha madhara...

MAPISHI: Drop scones

adminleo