Habari Mseto

Mkataba wa kusimamia bandari wapingwa mahakamani

July 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA PHILIP MUYANGA

CHAMA cha Makuli (DWU) kimewasilisha kesi mahakamani, kupinga makubaliano baina ya Serikali Kuu na kampuni ya kigeni kusimamia oparesheni katika bandari ya Mombasa.

Chama hicho kikishirikiana na Taireni Association of Mijikenda na shirika la kutetea haki za kibanadamu la Muhuri, kinahoji kuwa makubaliano hayo kati ya Serikali Kuu na kampuni ya Mediterranean Shipping Company (MSC) ni kinyume cha Katiba.

Wanasema kuwa kubinafsishwa kwa eneo hilo la makasha bandarini ni kinyume cha maadili ya uhuru wa Kenya kwa kuwa bandari ni mali ya taifa.

Wanaongeza kuwa mkataba huo wa kuhamisha oparesheni katika eneo hilo la bandari kwa kampuni ya kibinafsi haufai na utakuwa na matokeo mabaya kwa Wakenya.

“Mkataba huo umekumbwa na usiri mkubwa na pia serikali imekosa kufanya mikutano ya majadiliano na wananchi,” nakala za kesi hiyo zinaeleza.

Mkataba wa kusimamia eneo hilo mpya la mizigo bandarini uliwekwa saini wiki iliyopita kwenye hafla iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Awali wabunge kutoka Pwani na mabalozi kadhaa walikuwa wamepinga ubinafsishaji huo

Walalamishi wanasema mkataba huo hauna uwazi na kwamba raia hawakuhusishwa ama kupewa nafasi ya kueleza maoni yao.

“Mkataba huo ungefaa kuchapishwa na kuwekwa kwa wananchi ili waweze kuwa na nafasi mwafaka ya kujadili kwa kuwa eneo hilo la bandari linawahusu,” nakala za kesi zinasema.

Wanasema kuwa waliandika barua kwa serikali wakitaka ufafanuzi kuhusu mkataba huo lakini hawakujibiwa.

Walalamishi hao pia wanahoji kuwa kuna hatari ya watu wengi kupoteza kazi kwa sababu ya ubinafsishaji huo.

Wanataka agizo la muda kutolewa na mahakama kwa sasa la kusimamisha utekelezaji wa mkataba huo wakati kesi inapoendelea kusikizwa na kuamuliwa.

Korti inatarajiwa kutoa maagizo kuhusu ombi hilo.