Baraza la Agikuyu lamtaka Raila aendelee kuikosoa serikali
Na MWANGI MUIRURI
BARAZA la Agikuyu Jumamosi liliidhinisha umoja wa kinara wa NASA Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta lakini likamtaka Waziri huyo Mkuu wa zamani aendelee kukosoa serikali ili kulinda mali ya umma.
Lilimtaka Bw Odinga asilegeze wajibu wake wa kuhakikisha serikali ya Jubilee inatekeleza uongozi bora na kuwa rasilimali za Wakenya ziko salama.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Wachira Kiago akiongea Mjini Murang’a alisema kuwa uhasama wa kisiasa na kuendelezwa kwa hisia za utengano wa kijamii ni hatari kwa kila safu ya uhai wa taifa hili.
Alisema kuwa mazingira mwafaka ni ambapo kila mtu ana uhuru na uwezo wa kuongea na mwenzake kuhusu ufanisi na changamoto za taifa hili wala sio ile hali ya jamii kuwajibikia utengano kwa msingi wa kisiasa.
“Ni msimamo wetu kuwa Rais Uhuru Kenyatta sio rais wa Mlima Kenya au wa Rift Valley. Ukiangalia takwimu za upigaji kura katika chaguzi za Agosti 8, 2017 na Oktoba 26, 2017, utapata kuwa alipata kura kutoka maeneo yote ya hapa nchini hivyo basi kumpa sura ya kiongozi wa kitaifa,” akasema.
Kwa usajili huo pia, alisema kuwa ukiangalia takwimu za uchaguzi wa Agosti 8, 2017, utapata kuwa Odinga alipata kura kutoka kona zote za hapa nchini hivyo basi kumgeuza kuwa kiongozi wa kitaifa wala sio wa maeneo ambayo huorodheshwa kuwa ngome za upinzani.