• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Knut yashiriki mjadala kuhusu mtaala mpya

Knut yashiriki mjadala kuhusu mtaala mpya

PETER MBURU, OUMA WANZALA na WINNIE ATIENO

CHAMA cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kimelegeza msimamo wake na kushiriki kwenye mazungumzo ya wadau kuhusu mtaala mpya wa elimu (CBC).

Hatua hiyo ilichukuliwa jana wakati Serikali ilianzisha rasmi mazungumzo ya kitaifa ili kupokea maoni kutoka kwa Wakenya, kuhusiana na jinsi mtaala mpya wa elimu unafaa kutekelezwa.

Zoezi hilo lilianzishwa kwa hafla zilizoongozwa na maafisa wakuu serikalini katika maeneo manane, hafla kuu ikiongozwa na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha katika Kaunti ya Nakuru.

Katibu Mkuu wa Knut, Bw Wilson Sossion aliamrisha maafisa wake kote nchini kushiriki mazungumzo hayo, ili kuwapa walimu nafasi ya kutoa mchango wao kuhusu wanachotaka kifanywe wakati wa utekelezaji wa mtaala wa CBC.

Awali, muungano huo ulikuwa umetishia kutoshiriki mazungumzo hayo.

“Tutashiriki ili kuambia taifa kuwa mtaala mpya hautafaulu ikiwa hatua zifaazo hazitafuatwa,” akasema Bw Sossion, na kuongeza kushiriki kwao si kumaanisha wameidhinisha mtaala uendelee kutekelezwa jinsi hali ilivyo.

Katika hotuba yake, Prof Magoha aliendelea kushikilia msimamo mkali kuwa serikali haitashurutishwa kufuata malengo ya kibinafsi ya watu bali wizara itachukua maoni ambayo itaona yanaisaidia.

“Jinsi niliumbwa na Mungu namuamini yeye peke yake, hakuna mtu mwingine naamini. Ukiona nikitetea mtaala mpya ni kwa kuwa nimeenda shuleni na kuona jinsi unafunzwa, msiskize manabii wabaya wanaosema kuwa umefeli,” akasema Prof Magoha.

Licha ya kukiri kuwa kuna changamoto za kimiundomsingi katika shule nyingi za msingi nchini na tofauti kati ya idadi ya walimu na wanafunzi, waziri huyo alisema hilo halitazuia utekelezaji wa mtaala huo.

Prof Magoha alisema kuna baadhi ya shule ambapo mwalimu anafunza hadi wanafunzi 80, lakini akasema hilo halijaathiri shughuli za kufunza. Aidha, alisema serikali imetenga Sh300 milioni za miundomsingi shuleni, kutokana na changamoto kubwa iliyopo.

“Tutasikiza maoni yote na kuchukua yale yatakayotupeleka katika upande ufaao,” waziri huyo akasema.

Watu wengi ambao wamekuwa wakikosoa jinsi mtaala mpya wa elimu unatekelezwa, wamekuwa wakitilia shaka hali ya miundomsingi shuleni pamoja na tofauti baina ya idadi ya walimu na wanafunzi, mambo ambayo waziri alikiri ni changamoto zinazoshuhudiwa.

“Kuna changamoto kuhusu miundomsingi katika shule za msingi lakini serikali inazishughulikia,” akasema Prof Magoha.

Kwenye kikao kilichofanywa Mombasa, Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) Nancy Macharia alisema walimu 225,000 watakuwa wamepokea mafunzo kuhusu mtaala mpya kufikia Desemba.

You can share this post!

Mganga aonya pasta kwa kumchomea biashara

WAKILISHA: Atumia muziki kunyosha jamii

adminleo