• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
WAKILISHA: Atumia muziki kunyosha jamii

WAKILISHA: Atumia muziki kunyosha jamii

Na PAULINE ONGAJI

ANATUMIA muziki kuangazia masuala yanayoikumba jamii yake na katika harakati hizo kusaidia kupata suluhu.

Ni kazi ambayo Benjamin Kisentu, 24, msanii wa nyimbo za injili kutoka eneo la Kajiado, amekuwa akiifanya kwa miaka minne sasa huku akitumia lugha ya Kimaasai kupitisha ujumbe wake.

“Nia yangu ya kuimba kwa lugha hii kwa sasa ni kufikisha ujumbe wangu mashinani hasa katika maeneo ambayo lugha zingine bado hazitumiki,” asema.

Kufikia sasa ana nyimbo nne ikiwa ni pamoja na Keishu Olaitoriani, Keyiolo, Kashipakino na Ole Tipat Yetu.

“Nyimbo zangu hasa zinahusumasuala ya imani huku zikigusia mambo yanayoikumba jamii yetu kama vile ndoa za mapema na ukeketaji,” aeleza.

Azma yake ni kutunga nyimbo zitakazobadilisha maisha ya watu na kuwapa motisha wa kupambana na magumu na changamoto za maisha.

“Nia yangu pia ni kubadilisha mtazamo wa watu wengi wa jamii yangu hasa kuhusu tamaduni zinazoturudisha nyuma,” aeleza.

Na bila shaka mtazamo huo umemzolea mashabiki sio haba kwani amekuwa akipata mialiko mingi ya kufanya shoo na kujipatia donge nono pia. Aidha anajiundia pesa kutoka mtandao wa Skiza tunes.

“Fedha hizi nimeweza kusaidia familia yangu nazo na kufanya maendeleo mbalimbali nyumbani. Pia, nimeweza kujijengea makazi huku mipango zaidi ya kujistawisha ikiwa njiani,” asema.

Mbali na hayo, kipaji chake kimempa fursa ya kusafiri katika sehemu tofauti nchini na kumkutanisha na baadhi ya maafisa wakuu serikalini, miongoni mwao, Gavana wa sasa wa Kajiado, Joseph Ole Lenku.

“Pia, nimekuwa nikitumbuiza katika hafla mbalimbali kama vile harusi, ambapo mbali na kuniongezea kipato, kumenizidishia umaarufu,” aeleza.

Lakini hatumii muziki tu kujinufaisha kwani uimbaji umempa jukwaa la kuwanasihi vijana. Kwa mfano, Februari mwaka huu alizuru makao ya watoto ya Vijiji eneo la Kajiado.

“Mimi hasa huhimiza wanafunzi kutia bidii na kuafikia wanayotaka maishani,” asema.

Mzaliwa wa Kajiado, Kisentu alisoma katika shule ya msingi ya Isinya kisha baadaye akajiunga na shule ya upili ya Mashuru, na baadaye Chuo Kikuu cha St. Paul’s ambapo alisomea Uanahabari.

“Baada ya kupata kiwango fulani cha masomo, nilianza kuona mapengo yaliyokuwa yakisababishwa na baadhi ya tamaduni za jamii yangu,” asema.

Ajitosa katika ulingo wa muziki

Anaeleza kwamba haingekuwa rahisi kuikosoa jamii yake kwa kutumia elimu yake pekee, na hivyo mwaka wa 2015 alijitosa kwenye tasnia ya muziki kupitisha ujumbe wake.

“Jamii yangu inajulikana kwa kuhifadhi sana tamaduni zake. Hata hivyo, kuna baadhi ya itikadi zinazoturudisha nyuma kimaendeleo ambapo mara nyingi ni vigumu kushawishi watu kuhusu athari hizi. Lakini niliona muziki kama jukwaa ambalo lingekumbatiwa zaidi,” aeleza.

Anatumai kwamba katika siku zijazo, muziki wake utakuwa jukwaa kuu la kubadilisha mtazamo wa jamii nyingi kuhusu mambo yanayowarejesha nyuma.

You can share this post!

Knut yashiriki mjadala kuhusu mtaala mpya

MAPOZI: Bensoul

adminleo