Makala

AUNTY POLLY: Nitajuaje taaluma itakayonifaa?

July 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PAULINE ONGAJI

NATARAJIWA kukamilisha elimu ya shule ya upili mwaka huu 2019, suala ambalo limekuwa likinikosesha usingizi, hasa inapowadia wakati wa kuchagua taaluma ninayotaka kufanya. Kwa muda mrefu sasa nimejaribu kutafuta taaluma nitakayosomea bila mafanikio. Kila mara najipata nikichanganyikiwa. Nifanyeje?

Marion, 18, Nairobi

Ni vyema kujua kwamba tayari unapanga maisha yako ya usoni. Chaguo la taaluma halipaswi kuwa chini ya msingi wa pesa unazotarajia kupata kutokana na kazi hii, bali penzi lako. Kumbuka kwamba utaendelea na taaluma yako kwa muda mrefu maishani.

Kumbuka kwamba kila kitu huanza na penzi. Unapogundua unachofurahia kufanya, basi ni rahisi kupata mwelekeo wa taaluma ipi unayotaka kufanya maishani.

Ili kujua taaluma inayokufaa, unapaswa kutafuta kitu unachokipenda. Aidha unapaswa kutambua nguvu na udhaifu wako kitaaluma.

Baada ya kutambua unachofurahia kufanya, vilevile nguvu na udhaifu wako, unapaswa kutilia maanani uhalisia wake.

Nikisema hivi namaanisha unafaa kujiuliza maswali kama vile, natarajia kuwa na mapato ya aina gani kwa kufanya taaluma hii? Taaluma hii ina ushindani wa aina gani? Na je, nina uwezekano upi wa kujiimarisha baadaye maishani?

Hatua ya tatu inahusisha kufanya utafiti kuhusu taaluma hii. Unapaswa kwenda mtandaoni au kuzungumza na wataalamu kujua zaidi kuhusu jambo ulilochagua kufanya.

Kwa kufanya hivi, utaweza kulinganisha taaluma tofauti na kukupa fursa zaidi kuchagua. Unaweza kutambua mafunzo yanayofaa vile vile viwango vya kufuzu unavyohitaji ili kukuthibitishia nafasi katika taaluma uliyochagua.

Aidha, kwa kufanya hivi utaweza kuchagua taaluma inayoambatana na uwezo wako kimasomo.

Zaidi ya yote unapaswa kukumbuka kwamba ungali mchanga kiumri, na japo ni vyema kuwazia taaluma, suala hili halipaswi kukunyima usingizi.

Bado una muda wa kufikiria kuhusu nini hasa unachotaka kufanya maishani, na jambo hili litafinyangwa na matukio maishani mwako.