Wanaume wengi hunitaka kimapenzi ili wanipe ajira ya uigizaji – Gladys Waithira
Na JOHN KIMWERE
NDIO anaelekea kutimiza miaka minne tangu aanze kujituma kwenye masuala ya uigizaji ambapo amepania kufikia hadhi ya filamu za Hollywood. Anasema ni ndoto aliyoiwazia tangu akisoma kwenye shule ya Gakarati, Kaunti ya Murang’a.
Anasema anataka kutinga hadhi ya mwigizaji anayetesa kwenye filamu za Hollywood, Mkenya Lupita Nyong’o. Hakika wahenga hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa walivyolonga kuwa ‘Vitu vya biashara havigombani.’
Kutana naye binti mwenye umbo la kutamausha, tabasamu ya kuvutia anayelenga makubwa. Je huyu ni nani? Gladys Waithira Mbau mwigizaji anayeibukia, ambaye kitaaluma amehitimu kwa shahada ya diploma kama mwana habari. Pia ni video vixen ambaye kwa sasa anasomea masuala ya ususi katika chuo cha Beauty Point jijini Nairobi.
Hayo tisa. Kumi ni mfanyi biashara ambaye huuza mavazi ya wanawake na viatu kupitia mtandao wa kijamii wa face book kwa jina ‘Sweet Fashions.’
”Bila kujipiga debe ninaamini ninacho kipaji tosha ninacholenga kukikuza ili kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo,” anasema na kuongeza kuwa ana matamanio ya kufika mbali katika sekta ya maigizo.
Anajivunia kushiriki kipindi cha ‘Centro Cinema’ na Things cia Gwitu (Vitu za kwetu) ambazo hupeperushwa kupitia Inooro TV na Mt Kenya TV tangu mwaka 2017 na 2018 mtawalia. Aliwahi shiriki kipindi maarufu cha ‘Vioja mahakamani’ kilichokuwa kinapeperushwa kupitia KBC Televisheni miaka iliyopita.
Kadhalika ameshiriki filamu za ‘Wendo nduri mihaka’ (Upendo hauna mipaka) na ‘Mwihoko’ (Imani) zilizopakiwa katika mtandao wa kijamii wa Youtube ndani ya mwezi mmoja uliyopita. Kwa jumla amefanya kazi na brandi kama Gods Work Production na Njovijo Production kati ya zingine.
Anadokeza kuwa angependa kupiga shughuli na wasanii wa hapa nchini kama Sarah Ndanu na Sarah Hassan ilhali kimataifa anatamani kushirikiana nao Mercy Johnson na Inn Ido wote wa filamu za Kinigeria ‘Nollywood.’
”Natamani kumiliki brandi yangu ili kusaidia waigizaji wa kike ambao hujipata njiapanda mikononi mwa maprodyuza mafisi, lakini mwanzo wa ngoma napania kujijenga kisanaa,” alisema na kuongeza kuwa angepeda kukuza vipaji vya wasanii wanaoibukia maana anafahamu madhila ambayo hupitia kwenye pilkapilka za kutafuta ajira.
Je, kipusa huyu hupitia pandashuka gani katika masuala ya uigizaji? ”Dah! kuwa mrembo huchangia milima na mabonde kwa wanawake wengi duniani.
“Mimi hupitia wakati mgumu maana wanaume wengi hunitamani niwe wapenzi nao kusudi nipate ajira ya uigizaji. Nakumbuka binafsi niliwahi kupoteza ajira mara tatu nilipigia chini matakwa ya mabosi wangu. Pia niliwahi fanya kazi na kuondoka mikono mitupu baada ya kukataa kushiriki ngono na bosi wangu,” alisema.
Kadhalika anasema malipo duni huwavunja moyo wanawake wengi na kujikuta wakishiriki matendo maovu wakisaka posho. Binti huyu anashauri wenzie wanaokuja kwenye gemu kujiheshima wala wasikubali kutumiwa visivyo ili kupata ajira.