Habari Mseto

Siwezi kutetewa na wakili wa kike, mshukiwa aambia korti

July 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MALUMBANO makali yalizuka Jumanne katika kesi ya mauaji ya wakili mtetezi wa haki za binadamu Willy Kimani pale mmoja wa washukiwa alipokataa kutetewa na wakili mwanamke Bi Nelias Mucera Kinyori.

“Sitaki kutetewa na wakili mwanamke. Kesi yangu naona inaendelea vibaya. Naomba korti iamuru kuteuliwe wakili mwanaume aniwakilishe,” alirai Peter Ngugi Kamau.

Hatua hii ya Bw Kamau kumtimua kazi wakili Kinyori ilishangaza wengi hata ikamshtua wakili mwenyewe.

Akisimama kizimbani, Bw Kamau alimweleza Jaji Jessie Lesiit, “sitaki kuwakilishwa na wakili mwanamke. Nataka serikali imteue wakili mwanamume kuniwakilisha hata kama ni wakili Sam Nyaberi.”

Bw Kamau aliyekuwa kachero alisema “siridhishwi na jinsi wakili Bi Nelias Mucera Kinyori anaiendeleza kesi hiii na anafaa kujiondoa mara moja.”

Matamshi hayo ya mshtakiwa yalimshtua Bi Kinyori ambaye kwa mshangao alisema, “hata mimi nimeshangaa na kuduwaa na hatua hii. Nilifika kortini nikiwa tayari kuendelea na kumwakilisha Peter kama nilivyokuwa nikifianya tangu Septemba 2016. Hatujafarakana ama kukorofishana na mteja wangu Peter.”

Wakili huyo akamweleza Jaji Lesiit, “Nilipoingia kortini mteja wangu  aliniita pale kizimbani na kunieleza ametosheka na huduma zangu na nikome kumwakilisha. Nataka kujiondoa katika kesi hii. Namtakia mema katika harakati za kujitetea.”

Bi Kinyori alisema katiba iwazi kwamba kila mshtakiwa awakilishwe na wakili anayependezwa naye.

Lakini wakili Fred Ojiambo anayewakilisha familia ya wakili Willy Kimani aliyeuawa Juni 23 2016 katika eneo lka Mlolongo na maiti yake ikatupwa mto Athi River sehemu ya Donyo Sabuk alisema “ hatua hii ya wakili kujiondoa ni njama za kuchelewesha kuamuliwa kwa kesi hii.”

Alisema familia ya marehemu Kimani , mteja wake Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri inasubiri kuona haki imefanywa.

Bw Ojiambo alidai sarakasi hii ni hatua ya kuifanya mahakama ichoke na kesi hii na kuitiupilia mbali.

“Mshtakiwa anatakiwa kujua sarakasi hii anayoleta haikubaliki kamwe kisheria. Kifungu nambari 50 cha katiba hakimruhusu kuchagua jinsia ya wakili atakayemwakilisha mbali ni kamati ya huduma za kisheria inayomteua wakili bila kujali ni mwanaume ama mwanamke,” Ojiambo.

Wakili huyo aliomba mahakama itenge siku ya kusikizwa kwa kesi hivi karibuni ikitiliwa maanani wiki mbili zilizotengewa kesi hii zimeyoyoma kwa vile wakili Cliff Ombeta anayewatetea washukiwa watatu amekuwa mgonjwa.

Akimjibu Bw Ojiambo Bi Kinyori alisema “ hajafanya njama yoyote na mshtakiwa (peter) kujiondoa katika kesi hii kwa lengo la kuichelewesha.”

“Ni dhana potovu kusema nimefanya njama kuchelewesha kesi hii. Nimepashwa na mteja wangu hanitaki katika kesi hii na nimejiiondoa,”alisema Bi Kinyori.

Jaji Lesiit alimruhusu Bi Kinyori kung’atuka kesini na kumweleza mshtakiwa , “ nitaijulisha kamati ya haki na sheria kwamba hutaki wakili mwanamke.”

Lakini korti ilimweleza sio lazima atengewe wakili mwanaume.

Peter ameshtakiwa pamoja na maafisa wa polisi wa utawala Fredrick Leliman, Stephen Cheburet, Sylvia Wanjiku na Leonard Maina Mwangi.

Jaji Lesiit aliamuru kesi hiyo itajwe Julai 24 ijulikane ikiwa wakili mwingine ameteuliwa kumwakilisha.Kesi imeorodheshwa kusikizwa kuanzia Oktoba 7 mwaka huu.