• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
‘Al-Shabaab’ alitaka kusafiri Syria kujiunga na ISIS, korti yaelezwa

‘Al-Shabaab’ alitaka kusafiri Syria kujiunga na ISIS, korti yaelezwa

Na BRIAN OCHARO

SERIKALI ya Kenya sasa imesema mshukiwa wa Al-Shabaab, Salim Mohamed Rashid alikuwa anaelekea nchini Syria kujiunga na kundi la ISIS alipokamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi jijini Mombasa.

Kupitia kwa hati ya kiapo ya kutaka Bw Salim Mohamed Rashid kunyimwa dhamana, Serikali inasema uchunguzi wa kina umebaini kuwa mshukiwa huyo alikuwa katika harakati ya kupanda ndege ya kuelekea Syria kujiunga na kundi hilo.

Kulingana na upande wa mashtaka,mshukiwa huyo angetumia ndege ya Ethiopian Airlines kupitia nchi ya Sudan.

“Kupitia taarifa ya kijasusi,mshukiwa anaaminika kuwa katika mawasiliano na watu ambao wana uhusiano na Al-Shabaab na ISIS.Tunahofia kuwa mshukiwa anaweza kosa kuhudhuria mahakama na kuendelea na safari zake za kuenda kujiunga na ISIS,” Konstebo Onesmus Kiema, ambaye anachunguza kesi hiyo aliiambia mahakama.

Bw Kiema alisema mashtaka yanayomkabili mshukiwa yana ghadhabu kali mno na pia kuiambia mahakama kutilia maanani visa vya uvamizi vya kigaidi ambavyo vimetekelezwa na kundi la Al-shabaab nchini.

Kwa sababu hiyo, polisi huyo wa kitengo cha kupambana na ugaidi (ATPU ) alimuomba Hakimu Mwandamizi, Bi Rita Amwayi kumnyima Bw Mohamed dhamana hadi kesi yake itakapokamilika.

Bw Kiema aliongezea kuwa taarifa zaidi ya kijajusi imebaini kuwa wakala wa mshukiwa wanaaminika kuwa na silaha hatari ambazo wananuia kutumia katika kuvamia maeneo yasiyojulikana humu nchini wakati wowote.

“Pia tunachunguza visa vinavyohusika na ugaidi nje ya nchi na kuna uwezekano kuwa akiwachiliwa kwa dhamana, mshukiwa anaweza kuingilia uchunguzi na ushahidi katika kesi hii na kuhujumu haki,” alisema.

Aliiambia mahakama kuwa uchunguzi kubaini wakala wa mshukiwa na maficho yao bado inaendelea na anaweza kuhujumu shughuli hiyo akiachiliwa kwa dhamana.

Mchunguzi huyo alisema kuwa baadhi ya vitu ambavyo mshukiwa alipatikana navyo vikiwa ni nguo,mswaki na vinginevyo vimepelekwa katika maabara ya serikali kwa uchunguzi zaidi na kuwa ripoti kuhusu vitu hivyo bado inatayarishwa.

Bw Mohamed ambaye amekuwa korokoroni tangu Mei 14, amekanusha mashtaka dhidi yake ikiwa ni pamoja na kuwa mwanachama wa Al-Shabaab.

Alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza, mshukiwa huyo alikanusha mashtaka dhidi yake na kuambia mahakama imuachilie kwa dhamana akisma mashtaka dhidi yake ni ya kuekelewa tu.

Kulingana na stakabadhi ya mashtaka, upande wa mashtaka unadai kuwa mshukiwa huyo pamoja na wenzake ambao hawajakamatwa, walipatikana kuwa mwanachama wa kundi haramu la Al-Shabaab.

Upande wa mashtaka unadai kuwa mshukiwa huyo alifanya makosa hayo mnamo Mei 12 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi.

Mshukiwa huyo anashtakiwa zaidi kwa kosa la kupatikana na vifaa vya kutengeneza vilipuzi.

Serikali inadai kuwa mshukiwa alipatikana na vifaa hivyo mnamo Machi 8, katika eneo la Ngomeni, Kaunti ya Kwale.

Lakini mshukiwa huyo kupitia kwa wakili wake, Bw Chacha Mwita amepinga madai kuwa alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi.

Aliiambia mahakama kuwa alikamatwa katika mahakama ya Shanzu alipokuwa akielekea nyumbani baada ya kuachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 katika kesi nyingine inayohusiana na hiyo.

You can share this post!

Yafichuka Uhuru alimtuma Ruto kwa Munya

GWIJI WA WIKI: Mufti Mutahi

adminleo