KimataifaSiasa

Huenda Raila akateuliwa Balozi Maalum barani Afrika

March 18th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WANJOHI GITHAE

NAIROBI, KENYA

HUKU maswali mengi yakiendelea kuulizwa kuhusu hatima ya kisiasa ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga baada ya kubuni ushirikiano na Rais Kenyatta, duru zinasema huenda atateuliwa balozi maalum wa barani Afrika.

Vilevile, kiongozi huyo wa NASA atalipwa malipo yake ya uzeeni kwa kuhudumu kama waziri mkuu kati ya 2008 hadi 2013.

Na imefichuka kuwa kamati ya ushirikishi inayoongozwa na Balozi Martin Kimani na Wakili Paul Mwangi imekuwa ikitalii haja ya kumtengea Bw Odinga afisi maalum.

Duru zinasema kuwa wameelekeza macho yao kwa jumba la Upper Hill ambalo gharama ya kulikodisha inalipiwa kwa pamoja na serikali na wafadhili.

Inasemekana kuwa Rais Kenyatta atakuwa akimtuma Bw Odinga kama balozi wake wa amani katika mataifa yanayokumbwa na misukosuko barani Afrika.

Wajibu huu umekuwa ukitekelezwa na marais wa zamani barani Afrika, lakini Kenya haijawahi kuukumbatia licha ya kuwa katika nafasi bora ya kufanya hivyo kama ilivyo nchini za Nigeria, Ghana na Afrika Kusini.

Marais wa zamani wa mataifa haya wamekuwa wakipewa majukumu ya kuongoza harakati za kuleta amani katika mataifa yanayokumbwa na mapigano.

Bw Odinga ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani anatambuliwa barani Afrika na inatarajiwa kwamba atawakilisha Kenya katika majukwaa kadha kimataifa.
Kama sehemu ya makubaliano kati yake na Rais Kenyatta, Bw Odinga atapokea malipo yake yote kulingana na Sheria ya Malipo ya Kustaafu kwa Naibu Rais na Maafisa Wakuu Serikalini.

Ingawa sheria hiyo inasema sharti mhusika agure siasa kabla kupewa malipo hayo wanasiasa wa mirengo yote miwili hawaamini kuwa Bw Odinga atakoma kujihusisha na siasa za nchini hii miaka ijayo.

“Tunafahamu historia yake katika siasa ndiposa tunachukua tahadhari. Tunamkaribisha kufanya kazi na Rais kwa maendeleo ya taifa hili lakini sharti aelewe kuwa Jubilee ina mipango yake ya kisiasa,” akasema Naibu Spika wa Seneti Profesa Kithure Kindiki.

Kindiki ambaye ni seneta wa Tharaka Nithi alifafanua historia ya Bw Odinga kama njia ya kuhimili kauli yake; akitoa mifano ya mapambano yake ya kisiasa na aliyekuwa mwenyekiti wa Ford Kenya na Rais Mstaafu Daniel Moi.