• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Shujaa kupigania ubingwa kwenye Victoria Falls Sevens

Shujaa kupigania ubingwa kwenye Victoria Falls Sevens

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara nne wa Raga za Afrika za wachezaji saba kila upande, Kenya, wamethibitisha kupigania taji la Victoria Falls Sevens nchini Zimbabwe mnamo Machi 24-25, 2018.

Vijana wa kocha Innocent Simiyu, ambao walifika fainali ya duru ya Vancouver Sevens kwenye Raga za Dunia mnamo Machi 11, wako katika orodha ya mataifa manane yaliyoalikwa na mabingwa wa Afrika mwaka 2000 na 2012 Zimbabwe.

Mataifa mengine yaliyoingia makala haya ya Victoria Falls Sevens ni Uganda, ambao ni mabingwa wa Afrika mwaka 2016 na 2017, Zambia, Swaziland, Morocco na Senegal.

Timu za Ufaransa na Hong Kong pia zimealikwa kuwania taji la Victoria Falls Sevens, ambalo Zimbabwe ilinyakua mwaka 2017 kwa kupepeta Namibia 24-7 katika fainali.

Kenya, Zambia na Uganda zitatumia Victoria Falls Sevens kujipima nguvu kabla ya mashindano ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Jumuiya ya Madola kusakatwa Aprili 13-15, 2018 nchini Australia.

Katika mashindano ya Jumuiya ya Madola, Kenya na Zambia zilitiwa katikia Kundi C pamoja na New Zealand na Canada. Uganda iko katika Kundi D linalojumuisha Fiji, Wales na Sri Lanka. Kundi A linaleta pamoja Afrika Kusini, Scotland, Papua New Guinea na Malysia nazo Uingereza, Australia, Samoa na Jamaica zinaunda Kundi B.

You can share this post!

Hatimaye Moraa awabwaga wapinzani Poland

Kiyara aunda milioni kwa muda wa saa mbili Taiwan

adminleo