Makala

BIASHARA MASHINANI: Siri ya vuno kubwa la nyanya ni mbegu, mkulima aungama

July 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

KILIMO ni kazi inayohitaji kujitolea kwingi na kuwa na uvumilivu ili kupata manufaa.

Bw Njiru Gachoki ni mkulima wa nyanya wa kupigiwa mfano kutoka eneo la Ngariama Kusini katika Kaunti ya Kirinyaga.

Njiru ni tegemeo kubwa kwa familia yake ya mke na watoto wawili.

Amefanya ukulima wa nyanya kwa miaka saba sasa na ukweli ni kwamba hana lolote la kujutia kwa maana kilimo chake kinamlipa vizuri.

Kila mara anapotaka kuanza upanzi, yeye huwa anatayarisha zaidi ya miche 20,000 ya nyanya anayoipanda katika shamba lake la kukodi la ekari mbili.

Katika idadi ya miche 10,000 kwa kila ekari, kwa kawaida asilimia 90 hufaulu kukua na kunawiri ipasavyo.

Kabla ya kuziteua mbegu za kupanda, Njiru hufanya uchunguzi wa kina kwa lengo la kuhakikisha kwamba zitakua vyema na hatimaye kumletea mazao bora yenye tija.

Kwa asilimia 10 ya miche ambayo huwa inafeli kukua katika kiasi cha shamba la ekari moja, yeye huhakikisha kwamba anasalia na miche ya ziada ya kuzibia mapengo ya mimea iliyonyauka wakati wa upanzi.

Kulingana naye, baadhi ya mbegu bora zaidi kwa minajili ya kilimo cha nyanya ni Mahindra TM 20, Milele F1 na Rambo F1 ambazo hufanya vizuri zaidi katika sehemu zisizofikiwa na jua kali au zile zinazopokea unyevu na nyuzi joto zisizozidi 16.

Nyanya hukuzwa kwa urahisi zaidi katika udongo usio na kiwango cha juu cha asidi, wenye kiasi cha PH 6.3 – 6.8. Anawashauri wakulima kuongeza kiasi kingi cha mbolea, hasa kutoka kwa mifugo, iwapo udongo wao hauna kiwango cha kutosha cha madini ya chokaa au matawi ya mimea yanapoanza kupoteza rangi ya kijani na kugeuka kuwa manjano.

Njiru hutumia mbolea ya chokaa ili kuwezesha ukuaji mzuri wa nyanya na pia huweka dawa za kuzuia magonjwa kama vile Tomato Blight na Garlic Rust.

Garlic Rust ni ugonjwa wa fangasi ambao ukivamia mmea mmoja ni rahisi sana kuenea katika shamba zima la nyanya.

Chembechembe za Rust hubebwa na upepo kutoka eneo moja hadi jingine. Ugonjwa huu unapoenea, utaona ungaunga wa kahawia kwenye majani ya mimea. Mbinu ya kuzima ugonjwa huu ni kuondoa majani yenye Rust pindi tu unapoyaona.

Mkulima huyu hukuza nyanya kwa kipindi cha misimu mitatu ambapo msimu mmoja huchukuwa muda wa jumla ya miezi mitatu na nusu hadi minne.

Wakati zinapokua na kuwa tayari kuvunwa, yeye huhakikisha anachuma nyanya ambazo zimegeuka rangi na kuanza kuwa nyekundu.

Katika siku za mwanzo za kuvuna, huwa anapata masanduku matano na kwa kawaida, yeye huvuna mara mbili ama tatu kwa wiki kadri siku za mavuno zinaposonga.

Shamba lake lina uwezo wa kuvunwa masanduku 50 hadi 60 kila siku na wakati mwingine 65 katika kilele cha mavuno.

“Huenda nikavuna masanduku haya sitini mara tatu,” anasema.

 

Mkulima Njiru Gachoki apanda nyanya katika shamba lake katika eneo la Mwea, Kaunti ya Kirinyaga. Picha/ Chris Adungo

Katika msimu wa kuvuna, huwa anakubaliana na mawakala kuhusu siku yenyewe ili wauziwe moja kwa moja na kusafirisha hadi sokoni siku iyo hiyo.

Wengi wa mawakala hawa husafirisha nyanya hizo katika masoko ya Nairobi na Meru.

Wakati mawakala hawapatikani na mazao shambani yako tayari, huwa anakodisha gari na kupeleka nyanya zake hadi katika masoko ya Githurai na Muthurwa jijini Nairobi.

Anasema kwamba anapofika sokoni, bidhaa hii hununuliwa na kuisha kwa siku moja.

Anapouza mazao yake shambani, anaweza kupata hela zaidi kwani huwa ni ishara kwamba hamna nyanya kwa wingi sokoni na ndiposa mawakala hujitahidi kutafuta bidhaa hii kutoka kwa wakulima wenyewe mashambani.

Huenda akauza nyanya zake kwa hadi Sh7,000 kwa sanduku moja shambani.

Hii huwa ni tofauti na wakati anajipelekea zao hili sokoni ambapo anaweza kuuza kwa bei ya kati ya Sh5,000 au Sh6,000 pekee. Sababu ni kwamba anapopeleka sokoni, hamna mawakala wengi wanaofika shambani, ishara kwamba kuna mazao mengi ya nyanya katika sehemu nyinginezo nchini.

Changamoto ambazo yeye hupitia wakati mwingine ni pale ambapo nyanya zinakuwa nyingi zaidi na huenda bei ikapungua mno. Wakati mwingine, mazao yanaweza kuharibikia sokoni.

Katika kila mwisho wa msimu, anaweza kupata kati ya masanduku 350 na 400 ya nyanya. Ina maana kwamba yeye ana uwezo wa kujipa hadi Sh2.8 milioni kwa msimu mmoja.