Ndama mwenye miguu saba azaliwa Nakuru
Na SAMUEL BAYA
WAKAZI wa kijiji kimoja Rongai, Kaunti ya Nakuru wamekumbana na tukio la kipekee Alhamisi baada ya ng’ombe kuzaa ndama mwenye miguu saba.
Ndama huyo aliyezaliwa katika boma la Bw Kipkorir Langat hata hivyo amekufa saa chache baada ya kuzaliwa.
Wakati wanahabari wamefika katika kata ya Umoja, wanakijiji walikuwa wakiendelea kumiminika ili kujionea.
Hata vijiji jirani kama kile cha Lusaka vimepata habari hizo zilizoenea kama moto jangwani.
Bw Langat amesema mtaalamu wa mifugo alikuwa amemhakikishia kwamba ng’ombe wake angezaa ndama wawili wa kawaida.
“Nilimnunua ng’ombe wangu aina ya ayrshire kutoka kwa mkulima eneo la Mang’u akiwa mlegevu lakini nikamlisha kisawasawa. Sikudhania angezaa ndama mwenye miguu saba,” amesema Langat.
Vilevile amesema mtaalamu aliyefanya utungaji wa mimba kisayansi – artificial insemination – alikuwa amemuambia ng’ombe huyo angezaa ndama wawili.
Bw Langat ni daktari katika zahanati ya GSU, Kabarak.
“Daktari amekuja asubuhi na akasema alikuwa ametambua hata mguu wa nane uliokuwa karibu kuchipuka, kumaanisha kwamba ndama wangekuwa pacha. Hata hivyo, kufikia sasa nimemlisha ng’ombe aliyezaa na anaendelea kupata nafuu, amesema Langat.
Mwenyekiti wa mpango wa Nyumba Kumi eneo la Umoja Bw Francis Langat, amewaambia wanahabari kweli ng’ombe huyo amezaa ndama mwenye kasoro za kimaumbile.
“Nilipata habari hizi kutoka kwa jirani Mary Njoki kwamba ndama wa aina hii alikuwa amezaliwa kwa boma la Dkt Langat,” amesema Langat.
Bi Njoki ambaye ni katibu wa Nyumba Kumi kijijini amesema naibu chifu alimtaka aende kwa Bw Langat kujionea kuhusu habari hizo.