• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:36 PM
Washirika wa Ruto Kakamega sasa wabadili wimbo

Washirika wa Ruto Kakamega sasa wabadili wimbo

BENSON AMADALA na GAITANO PESSA

WABUNGE kutoka Kakamega wanaoshirikiana na Naibu Rais William Ruto, wameanza kubadilisha msimamo wao kuhusu kuunga azma yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Matamshi ya hivi punde ya wabunge Emmanuel Wangwe (Navakholo), Bernard Shinali (Ikolomani, pichani) na Malulu Injendi (Malava) yanaonyesha kuwa wamebadilisha nia kuhusu suala hilo wakisema lengo lao kwa sasa ni kuhakikisha jamii ya Waluhya itakuwa kwenye serikali ijayo.

Walisema mgombeaji yeyote anayetaka kuungwa mkono eneo la magharibi anapaswa kujiandaa kujadiliana na viongozi wa jamii ya Waluhya.

Bw Wangwe alifichua msimamo wa wanasiasa hao kwenye kauli yake.

“Naibu Rais ni jirani yetu na rafiki lakini hakutakuwa na uungwaji mkono wa moja kwa moja wa azima yake ya urais iwapo hatutaweza kujadili jinsi jamii ya Waluhya itanufaika kwa kumuunga kupata urais.”

Dkt Ruto amefanya ziara kadhaa kaunti ya Kakamega kujipigia debe katika kile kinachoonekana kujenga umaarufu wake eneo hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Washirika wake kutoka eneo hilo ni pamoja na Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Emmanuel Wangwe (Navakholo), Bernard Shinali (Ikolomani), aliyekuwa waziri Rashid Echesa na aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale.

Akiongea katika kanisa Katoliki la Sabane eneo la Ikolomani Jumapili iliyopita, Bw Echesa alisema jamii ya Waluhya haitacheza kamari ya kisiasa kwa kumuunga mgombea urais asiyekuwa na ajenda ya maendeleo ya eneo hilo.

Alisema eneo hilo haliwezi kumudu kubaki kwenye baridi baada ya wapigakura kupotoshwa kuunga wagombeaji waliotumia jamii ya Waluhya kuingia mamlakani.

“Nimemwambia Musalia (Kiongozi wa chama cha ANC) arudi nyumbani ili tuanze kutafuta marafiki kutoka jamii nyingine ambao watamuunga mmoja wetu kushinda urais,” alisema Bw Echesa.

Lakini Dkt Khalwale alisisitiza kuwa jamii ya Waluhya inapaswa kumuunga Dkt Ruto kuhakikisha atashinda urais kwenye uchaguzi wa 2022.

“Hatutaki kutoa ishara mseto kuhusu uamuzi wetu wa kumuunga Naibu Rais kwa sababu ndiye yuko katika nafasi nzuri ya kushinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Tumuunge Naibu Rais ili jamii ya Waluhya iwe na sauti katika serikali ijayo,” alisema Dkt Khalwale.

Na katika kaunti ya Busia, uamuzi wa Gavana Sospeter Ojaamong, mbunge wa Teso Kusini Geoffrey Omuse na baadhi ya madiwani kutoka jamii ya Wateso wa kumuunga Dkt Ruto kugombea urais umeibua joto katika chama cha ODM.

Mwenyekiti wa tawi la Busia la chama cha ODM, Bw Patrick Obongoya, alisema kwamba chama kitawaita viongozi hao kueleza uhusiano wao na Dkt Ruto kabla ya suala hilo kupelekekwa kwa Baraza Kuu la Kitaifa.

“Hatujafurahishwa na baadhi ya matamshi ya gavana Ojaamong na Bw Omuse, ambayo yalionyesha wana njama fiche walipokutana na Naibu Rais Ruto,” alisema Obongoya ambaye pia ni diwani maalum.

Alisema katibu mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna tayari anafahamu hatua wanazopanga kuchukua.

Chama hicho kimewahi kuchukua hatua sawa na hiyo dhidi ya wabunge Suleiman Dori (Msambweni) na Asha Jumwa (Malindi), kwa kujihusisha na Bw Ruto.

You can share this post!

Aliyejichimbia kaburi miaka 17 iliyopita kuzikwa

Seneti yaishtaki Bunge la Kitaifa

adminleo