• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Vibarua wa bandarini kuongezewa malipo kutoka Sh250 hadi Sh1,500 kwa siku

Vibarua wa bandarini kuongezewa malipo kutoka Sh250 hadi Sh1,500 kwa siku

 ANTHONY KITIMO na PHYLIS MUSASIA

WAFANYIKAZI wa vibarua katika Bandari ya Mombasa wanatarajiwa kupata nyongeza ya malipo yao baada ya chama chao kutia saini mkataba wa utendakazi wao na wamiliki wa meli.

Mkataba huo unaotarajiwa kutekelezwa karibuni, utawasilishwa katika Mahakama ya Ajira na Leba wiki ijayo , abapo utaongeza mshahara wa wafanyakazi hao kutoka Sh250 hadi kati ya Sh1,000 na Sh1,500 kulingana na kitengo cha kazi.

Mwenyekiti wa muungano wa shirika la wanakandarasi nchini (KSCA), Bw Richard Jefwa alisema mkataba huo ni juhudi ambazo wamekuwa wakishinikiza muungano wa wamiliki wa meli nchini (KSA)kuukubali ili kuboresha maisha ya wafanyikazi hao.

“Wafanyikazi hao wamekuwa wakinyanyaswa na wamiliki wa meli na hawajaongezewa misharahara kwa muda wa miaka mingi ambayo ni kinyume na sheria za Kenya. Wiki ijayo itakuwa ni furaha kwa wengi na tutaomba mkataba huo uweze kutekelezwa mara moja unapowasilishwa katika mahakama ya Ajira na Leba nchini,” alisema Bw Jefwa.

Mwenyekiti huyo alisema zaidi ya wamiliki 45 wa meli watashurutishwa kubadili kandarasi na wafanyakazi hao ili uambatane na mkataba huo mpya.

“Kundi hilo la wafanyakazi hufanya kazi watu wanane kwa muda wa saa nane na hupokea takriban Sh1,250 kwa kila kundi. Hicho ni kiasi kidogo sana cha pesa kulingana na sheria zetu za nchi,” alisema Bw Jefwa.

Shirika la mabaharia nchini (SUK) pia limekuwa likiunga mkono mapendekezo hayo kwa kuwa wengi wa wafanyakazi hao hawajajiunga kwa vyama vya wafanyikazi, hali inayowakosesha mtetezi wa maslahi yao.

Mkataba huo utakapotekelezwa utakuwa ni wa pili kwa muda wa miaka miwili ili kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi hao yanashughulikiwa na waajiri wao.

Katika kaunti ya Nakuru, wafanyikazi 23 walioajiriwa kwa kandarasi wamelalamikia kucheleweshewa mshahara kwa miezi sita sasa.

Wafanyikazi hao ambao husafisha mji pamoja na soko ,walisema imekuwa vigumu kwao kutimiza majukumu yao binafsi.

You can share this post!

Seneti yaishtaki Bunge la Kitaifa

Huduma Namba: Waliodinda kujisajili kuadhibiwa

adminleo