De Ligt atua Juventus, ajibebea taji la beki ghali zaidi sokoni
Na MASHIRIKA
ROME, Italia
BEKI wa kati Matthijs de Ligt amempiku Mholanzi mwenzake Virgil van Dijk kutoka klabu ya Liverpool kama beki ghali duniani baada ya kujiunga na Juventus kutoka Ajax kwa ada ya Sh9.9 bilioni, miamba hao wa Italia walisema Alhamisi.
Chipukizi huyu mwenye umri wa miaka 19 amesaini kandarasi ya miaka mitano.
Juventus ilisema katika taarifa yake kuwa takriban Sh8.7 bilioni zitalipwa kwanza kwa kipindi cha miaka mitano. Italipia pia “gharama za ziada” za Sh1.2 bilioni.
Ada hii inafanya De Ligt kuwa mchezaji wa tatu ghali katika historia ya klabu ya Juventus baada ya mshambuliaji matata wa Ureno Cristiano Ronaldo kununuliwa kwa Sh12.1 bilioni kutoka Real Madrid mwaka 2018 na Sh10.4 bilioni ilizolipa Napoli kupata huduma za mvamizi wa Argentina Gonzalo Higuain mwaka 2016.
De Ligt alikuwa akimezewa mate na Manchester United, Barcelona na Paris Saint-Germain baada ya mchezo wake wa kuvutia kusaidia makinda wa Ajax kufika hatua ya nusu-fainali kwenye Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita wa 2018-2019.
Mchezaji mwenza Frenkie de Jong,22, ambaye ni kiungo amejiunga na miamba wa Uhispania, Barcelona.
De Ligt alisakata mechi 117 akivalia jezi ya Ajax katika mashindano yote akicheka na nyavu mara 13, na kupachika bao la ushindi mjini Turin wakati Ajax ilibandua nje Juventus kwenye Klabu Bingwa Ulaya katika robo-fainali.
Mchezaji huyu amesakatia Uholanzi mechi 17 akiunda ushirikiano imara katika safu ya nyuma na nyota wa Liverpool, Dijk.
Alitwikwa majukumu ya nahodha wa Ajax mnamo Machi mwaka 2018 na kuwa nahodha aliye na umri mdogo kabisa kuwahi kuhudumu kama nahodha wa klabu hiyo.
Mchango wa Ronaldo
De Ligt alifichua kuwa Ronaldo alichangia pakubwa katika uhamisho wake hadi Juventus alipomuomba ajiunge na miamba hawa wa Italia baada ya kukabiliana katika fainali ya Uefa Nations League mwezi Juni ambayo Ureno iliibuka mshindi.
De Ligt sasa amepiku Dijk aliyetua Liverpool kutoka Southampton kwa Sh9.7 bilioni na na Mfaransa Lucas Hernandez aliyejiunga na miamba wa Ujerumani Bayern Munich kwa Sh9.2 bilioni kutoka Atletico Madrid.
Akiwa Juventus, majukumu yake yatakuwa kuimarisha safu ya ulinzi ambayo ina wachezaji Leonardo Bonucci, 32, na Giorgio Chiellini, 34, wanaoingia katika mwaka wao wa mwisho katika taaluma yao na hasa, Chiellini ambaye majeraha yanamsumbua.
Juve pia imenunua mabeki wa kati Mturuki Merih Demiral, 21, kutoka Sassuolo na Cristian Romero, 21, ambaye amewasili kwa mkopo kutoka Genoa.