• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
Mwalimu ajitolea kutetea haki za watoto

Mwalimu ajitolea kutetea haki za watoto

NA RICHARD MAOSI

Bw Sigei Justice Kiprono amegonga vichwa vya habari kutokana na juhudi zake kupigania haki za watoto hususan wa kike chini ya mwavuli wa kampeni inayofahamika kama Child Protection.

Anasema tamaduni za kale na ukosefu wa uhamasisho wa kutosha kuhusu haki za binadamu, ndicho chanzo kikubwa cha kurudisha nyuma ndoto za watoto kupata mafanikio maishani.

Akiwa mwalimu katika Shule ya Msingi ya Kimari inayopatikana kaunti ya Bomet, alishirikiana na hospitali ya Nairobi Women kuchunguza na kabiliana na wale wanaokiuka haki za watoto.

Alieleza kuwa watoto wanastahili kulindwa dhidi ya taasubi za kiume ili kuhakikisha maisha yao hayamo hatarini kwani sheria inawalinda.

Sigei anasema walilenga kufundisha jamii namna mbalimbali za kukiuka haki za mtoto,mbali na kuwapatia wanafunzi ujuzi wa kujitegemea kimaisha.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, alisema kwanza alibuni makundi ya kuigiza shuleni yanayotumia mashairi na nyimbo kuhamasisha jamii.

Bw Sigei Justice Kiprono. Picha/ Richard Maosi

Hatua yenyewe ilimsaidia kuvutia idadi kubwa ya wanafunzi, ikizingatiwa wao huchukua muda mfupi kujifunza kitu kipya muradi kitawafurahisha.

Katika mradi huo alijaribu kuhimiza wanafunzi,wake na walle wa shule jirani kutumia elimu wanayopata shuleni kuimarisha nidhamu kwenye makuzi yao ya kila siku.

“Tangu Gender Violence Recovery Centre kuchukua usukani visa vya ukiukaji wa haki za watoto katika kaunti za Kericho na Bomet vimepungua kwa asilimia kubwa,” akasema.

Aidha amefanikiwa pamoja na washikadau kuwawezesha watoto kupata elimu na ufadhili ili wasikatize masomo yao wakiwa njiani,kabla ya kujitimu na kupata cheti.

Sigei anasema hususan mtoto wa kike amekuwa kwenye hatari zaidi kutokana na mimba za mapema au ubakaji.

Lakini hata hivyo anawalaumu wazazii kwa kuwasukumia walimu jukumu hilo na badala yake kutumia wakati wao mwingi wakifanya kazi.

Anapendekeza wazazi kuwapatia watoto wao pesa za kutosha kwa sababu ya mahitaji ya kila siku,kwani hali ngumu ya maisha inaweza kuwasukuma watoto kwa utumiaji wa mihadarati.

Akitoa mfano katika eneo la pwani ambapo visa vya ulanguzi wa watoto vimekuwa vikiongezeka kutokana na mfumo mpya wa teknolojia na utandawazi.

Biashara hiyo imechangiwa na mitandao ya kijamii kwa asilimia kubwa na wazazi hawajakuwa wakichukua jukumu la kuangalia watoto wao wanazungumza na akina nani kwenye mitandao.

“Ulanguzi wa binadamu hasa watoto umekuwa ukiongezeka kutokana na mahitaji ya kimaisha kama vile umaskini na idadi kubwa ya vijana wanaotafuta ajira mtandaoni,”akasema.

Pia walezi wamekuwa wanyonge na woga hasa ijapo katika swalla la kuwaelimisha watoto kushiriki mapenzi wakiwa wachanga.

Sigei aliteuliwa kama mwenyekiti anayesimamia kaunti ya Bomet na Kericho kama balozi atakayepitiza ujumbe kuhusu haki za watoto na maeneo mengineyo Bonde la ufa.

Akiwa mwalimu amefanikiwa kufikia familia nyingi hasa mashinani ambao awali hawakuona umuhimu wa kuwapeleka watoto wao shuleni.

Aidha kutokana na ushawishi wake amepigana na tamaduni zilizopitwa na wakati na akafanikiwa kuonyesha kuwa mtoto wa kike ni sawa na mtoto wa kiume.

Kwa ushirikiano na usimamizi wa shule ya Kimari walifanikiwa kubuni chama cha Kings and Queens ambacho kinawahimiza wanafunzi wazifahamu haki zao za kimsingi.

Kings and Queens

Kings and Queens ni kikundi cha wanafunzi wenye ndoto za kuja kuwa watu wa maana katika jamii siku za mbeleni,hivi sasa wakiwa wanafunzi 41 maaazimio yao ni ya kutia moyo.

Mwalimu Sigei alitaka kuwaleta pamoja wanafunzi kutoka tabaka la juu na tabaka la chini na kuwaonyesha jinsi masomo yangeweza kuwaunganisha wawe sawa.

“Ni kupitia elimu tu ambapo jamii itafanikiwa kupigana na chagamoto zinazomkabili mtoto,”aliongezea.

Brenda Chepkoech ni mwanafunzi wa darasa la nane,anasema yeye ni mshiriki wa michezo ya kuigiza ambapo anatumia kipaji chake kuhimiza maadili miongoni mwa wenzake.

Anawashauri watoto wengine kutafuta msaada wa haraka endapo watagundua maisha yao yako hatarini.

“Wanafunzi wengi wanazingatia ushauri wa kufanya kazi kwa bidii ili kujitengenezea maisha yao ya siku za mbeleni,”aliongezea.

Ni kwa sababu hiyo kupitia serikali ya ugatuzi wizara imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa mtoto wa kike haponzwi na taasubi za kiume.

Ambapo sheria inatoa utaratibu dhidi ya ukiukaji wa haki za mtoto akiwa mdogo,aidha sheria inaunga mkono ajenda ya kulinda maslahi ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa kwani wana haki ya kurithi mali ya wazazi wao.

You can share this post!

Kuria ajiona kama ‘zawadi’ kwa Wakenya

Serikali kukagua wanaume kubaini ikiwa wametahiriwa

adminleo