'Punguza Mizigo' yagawanya wanasiasa
Na WAANDISHI WETU
MSWADA wa kurekebisha katiba unaotarajiwa kuwasilishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa mabunge ya kaunti, Jumapili ulizidi kuibua hisia mseto miongoni mwa viongozi wa kisiasa.
Hayo yamejiri huku Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga miongoni mwa wengine wakisalia kimya kuhusu pendekezo hilo.
Wabunge, maseneta na madiwani katika maeneo mbalimbali wametofautiana, kwani baadhi yao wanaunga mkono mswada huo uliofadhiliwa na Chama cha Thirdway Alliance kinachoongozwa na Dkt Ekuru Aukot, lakini wengine wanapinga vikali.
Vigogo wa kisiasa katika Chama cha ODM walipuuzilia mbali mswada huo na kusema mchakato pekee wa marekebisho ya katiba ambao wanatambua ni ule unaoendeshwa na jopokazi la maridhiano (BBI).
Kwa upande mwingine, kuna mgawanyiko katika Chama cha Jubilee kwani imeibuka wandani kadhaa wa Naibu Rais William Ruto wanaunga mkono mswada huo, ilhali viongozi wengine chamani wanaupinga.
Viongozi wa ODM wakiwemo Wabunge Otiende Amolo wa Rarieda na Opiyo Wandayi wa Ugenya, pamoja na seneta wa Siaya James Orengo waliwataka wafuasi wao kupuuzilia mswada huo wa Dkt Aukot, na badala yake wasubiri pendekezo litakalotolewa na jopokazi la BBI lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga, walipoweka mwafaka wa maelewano mwaka uliopita.
“Refarenda tunayotambua ni itakayoletwa na Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga baada ya ripoti ya BBI. BBI ndiyo itatoa ripoti kuhusu uongozi wa nchi,” akasema Bw Orengo.
Wakiunga mkono pendekezo la Dkt Aukot, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen na mbunge maalum David Ole Sankok walio wandani wa Dkt Ruto, walisema mapendekezo hayo yatamfaa mwananchi.
Kulingana na Bw Murkomen ambaye ni seneta wa Elgeyo Marakwet, huu ndio wakati wa madiwani kuonyesha mamlaka yao kwa kuupitisha mswada huo, akisema wamekuwa wakipuuzwa.
“Waupitishe ili kuwakumbusha watu kuwa ugatuzi una maana,” akasema seneta huyo.
Lakini Kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale aliwaonya madiwani Kaunti ya Garissa kutopitisha mswada huo, akisema wataadhibiwa na wakazi wakiupitisha.
Bw Duale aliapa kuhakikisha mswada huo hautapita punde tu ukiwasilishwa katika mabunge ya kaunti.
“Tutazungumza na MCAs wa eneo pana la kaunti kame ili zisipitishe mswada wenyewe. Tutaupinga ili kuhakikisha haufikishi kaunti 24,” Bw Duale akasema.
Katika eneo la Kati, Wabunge Munene Wambugu kutoka Kirinyaga ya Kati, Gichimu Githinji wa Gichugu na Kabianga Wathayu wa Mwea nao walisema kuwa mswada huo hautawafaa Wakenya wa kawaida, wakisema unafaa kubadilishwa.
Viongozi hao walikuwa wakizungumza katika kanisa la Presbyterian katika Kaunti ya Kirinyaga, ambapo walisema mswada huo unafaa kupitishiwa kwa wananchi kwanza watoe maoni kuuhusu, kabla ya kufikishwa katika mabunge ya kaunti.
“Mswada huo ukiletwa bungeni jinsi ulivyo, mimi siutauunga mkono. Wakenya wanafaa kutoa maoni yao kwanza,” akasema Bw Wambugu.
Magavana John Lonyangapuo wa Pokot Magharibi na mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto pia walimkosoa Dkt Aukot, pia walipuuzilia mbali mswada wake kuwa usio na maana yoyote.
Gavana Lonyangapuo alisema kuwa Dkt Aukot anasukuma mswada huo akiwa na lengo la kujinufaisha kisiasa, akidai kuwa kiongozi huyo wa Third Way Alliance analenga kuwa Gavana wa Turkana katika uchaguzi mkuu ujao.
“Tunajua kuwa analenga kuwa gavana hivyo aache kuwadanganya Wakenya,” akasema Prof Lonyangapuo.
Bw Moroto naye alisema kuwa japo kuna haja ya kufanya mabadiliko ya kikatiba, baadhi ya mapendekezo ya Dkt Aukot hayawezekani na kuwa kuna mengine ambayo hajajajumuisha.
“Tunaunga mkono mambo kama mawaziri kuteuliwa kutoka bungeni kwani viongozi wa kuchaguliwa ndio wanafahamu shida za wapiga kura, kinyume na wale wanaotolewa kutoka nje ya bunge,” akasema mbunge huyo.
Lakini mbunge huyo alipinga pendekezo la mswada huo la kupunguza idadi ya maeneobunge, akisema halifai.
Habari za George Munene, Oscar Kakai, Justus Ochieng, Rushdie Oudia Na Vitalis Kimutai