• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
REFERENDA: Duale atoa sababu ya kuanguka kwa mswada wa tarehe mpya ya uchaguzi

REFERENDA: Duale atoa sababu ya kuanguka kwa mswada wa tarehe mpya ya uchaguzi

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA sasa wataendelea kushiriki uchaguzi mkuu mwezi Agosti kila baada ya miaka mitano kufuatia kuangushwa kwa mswada ambao ulikuwa umependekeza tarehe hiyo ibadilishwae hadi Desemba.

Mswada huo ambao ulidhaminiwa na Mbunge wa Kiminini, Chris Wamalwa ulikuwa unataka uchaguzi mkuu uwe ukifanyika Jumatatu ya tatu mwezi Desemba badala ya Jumanne ya pili Agosti.

Mswada huo ulianguka Oktoba 17, 2018 alasiri baada ya wabunge 187 pekee kuhudhuria kikao, ilhali wabunge 233 ndio waliohitajika kuunga mkono.

Ikiwa mswada huo ungeungwa mkono na wabunge 233 au zaidi, muda wa kuhudumu kwa Rais Uhuru Kenyatta ungeongezwa kwa miezi minne.

Wabunge pia wangeendelea kuwa afisini kwa kipindi hicho hicho.

Hii ina maana kuwa walipa ushuru wangegharamia mishahara ya ziada ya wabunge ya kima cha Sh1.2 bilioni ikizingatiwa kuwa kuna jumla ya wabunge na maseneta 416.

Hii ni kando ya gharama ya mishahara na marupurupu ya jumla ya madiwani 2,250 ambao pia wangefaidi kutokana na kusongezwa kwa tarehe ya uchaguzi.

Bw Wamalwa alitetea pendekezo lake akisema kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwezi Agosti kutaathiri kalenda ya masomo n ahata mitihani ya kitaifa, endapo uchaguzi wa urais utarudiwa kama ulivyofanyika mwaka jana.

Vile vile, alisema kuwa tarehe ya Agosti itaathiri kusomwa kwa bajeti ya kitaifa ambayo hufanyika sambamba na mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Baada ya kufeli kwa mswada huo kiongozi wa wengi Aden Duale alisema hiyo ilitokana na sababu kwamba Bw Wamalwa hakuwashiwi wabunge wenzake vizuri, haswa uongozi wa mirengo miwili, Jubilee na NASA.

“Tangu mjadala kuhusu mswada huu ulipokamilika wiki iliyopita, Bw Wamalwa hajakuja afisini mwangu kuomba usaidizi. Sidhani ikiwa alimfikia kiongozi wa mrengo wake Bw John Mbadi,” akasema.

Mbunge huyo wa Garissa Mjini alisema hata wabunge 187 waliokuwa bunge “wengi wao walipinga kubadilishwa kwa tarehe ya uchaguzi.

“Hata hivyo, nampongeza Bw Wamalwa kuwa jasiri kuleta mswada kama huu,” akasema.

Bw Wamalwa alijitetea akisema kuwa japo amevinjika moyo baada ya mswada wake kuanguka alifurahi kwamba aliweza kuteleza wajibu wake kama mbunge.

“Naamini kuwa watu wangu wa Kiminini pia wamefurahi kwamba walichagua kingozi ambaye anafahamu wajibu. Na bila shaka mwaka wa 2022 wataniunga mkono nitakapowania ugavana wa Trans Nzoia,” akasema Bw Wamalwa.

You can share this post!

GHARAMA YA MAISHA: Bei ya stima kupanda tena huku Safaricom...

Utakuwa mlima kwa Ruto kupenyeza magharibi – Wandani...

adminleo