• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:58 PM
Hisia mseto kuhusu ‘Punguza Mizigo’

Hisia mseto kuhusu ‘Punguza Mizigo’

NA WAANDISHI WETU

MADIWANI wa Mabunge ya kaunti za Kaskazini mwa Bonde la Ufa wameapa kuunga mkono mswada wa Punguza Mizigo unaodhaminiwa na Kinara wa chama cha Third Way Alliance Dkt Ekuru Aukot, wakisema unatilia maanani maslahi ya raia.

Madiwani hao kutoka Kaunti za Baringo, Uasin Gishu, Nandi, Pokot Magharibi na Elgeyo-Marakwet jana walisema Muungano wa Mabunge ya Kaunti Nchini utaunga mkono mswada huo na kupendekeza marekebisho machache kabla ya kuupitisha.

“Wakenya wameumia kwa muda mrefu kwa sababu kuna mambo ambayo yapo kwenye Katiba yanayochangia mateso yao. Kuna baadhi ya nyadhifa za kisiasa kama Bunge la Seneti na Mwakilishi wa Kike ambazo zinatekeleza majukumu sawa na zinafaa kufutiliwa mbali,” akasema diwani wa wadi ya Silale, Kaunti ya Baringo, Nelsom Lotela.

Spika wa bunge la kaunti ya Uasin Gishu, Bw David Kiplagat, alisema mabunge yote eneo la Bonde la Ufa yatatoa msimamo wao kamili kuhusu mswada huo, lakini akasema tayari umewaridhisha.

Katika kaunti ya Baringo, diwani mteule Francis Kibai alisifu kubuniwa kwa hazina ya wadi, akisema itasaidia kufikisha maendeleo kwa raia mashinani.

“Mswada huu unapendekeza kuwe na hazina ya wadi na kuongeza fedha za ugatuzi kutoka asilimia 15 hadi 35. Ongezeko hilo litanufaisha wananchi na tunaliunga mkono,” akasema Bw Kibai.

Mwenyekiti wa kamati ya Elimu katika bunge la kaunti ya Nandi, Bw Emmanuel Mengich (wadi ya Lessos) na mwenzake wa wadi ya Terik Osborne Komen, waliunga pendekezo la kuondoa wadhifa wa mwakilishi wa kike.

Wabunge William Kamket (Tiaty) na Janet Sitienei (Turbo) hata hivyo walitofautiana kuhusu mswada huo, Bw Kamket akiuunga naye Bi Sitienei akiupinga.

“Japo naunga mswada huo, napinga kufutiliwa mbali kwa baadhi ya maeneo bunge kwa sababu wabunge ni wawakilishi wa raia,” akasema Bw Kamket.

Kinara wa Ford Kenya Moses Wetang’ula naye akizungumza mjini Nakuru alipinga mswada wa Dkt Aukot akisema yaliyomo yanafaa kujumuishwa na mapendekezo yatakayotolewa na kamati ya uwiano (BBI) kisha yawasilishwe kwa Wakenya kupitia kura ya maamuzi.

Ripoti za Wycliff Kipsang’, Tom Matoke, Florah Koech, Evans Kipkura, Geoffrey Ondieki na Oscar Kakai.

You can share this post!

Kibarua adungwa kisu alipofumaniwa na mke wa mtu kitandani

Picha pekee hazitoshi kuthibitisha uko kwa ndoa –...

adminleo