Habari Mseto

Picha pekee hazitoshi kuthibitisha uko kwa ndoa – Mahakama

July 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOSEPH WANGUI

MAHAKAMA Kuu imetoa uamuzi kuwa mwanamume na mwanamke hawawezi kutumia picha zao wakiwa pamoja kuthibitisha kuwa mume na mke.

Jaji Florence Muchemi jana aliamua kuwa picha za aina hiyo zinaweza kutumiwa kueleza hadithi kuhusu watu na uhusiano wao, wala haziwezi kuwa ushahidi utakaokubaliwa na korti.

Alisema hivyo alipokuwa akitoa uamuzi katika kesi ambapo mwanamke na mamake wa kambo walikuwa wakizozania shamba, baada ya babake mwanamke huyo kufariki.

Irene Waithira ambaye alidai kuwa alikuwa mke wa marehemu Njeru Njagi alionyesha korti picha 13 zake na marehemu kama ushahidi wa pekee kuwa walikuwa wameoana na marehemu.

Lakini Bi Annete Wandia, bintiye marehemu alipinga vikali akisema Bi Waithira hakuwahi kuwa mke wa babake, na kusema hawakuwa na uhusiano wowote.

Aliiomba korti kufutilia mbali nakala zilizompa mamlaka ya kumiliki mashamba ya babake, akisema hakuwa mkewe. Alisema hata babake alipokufa, Bi Waithira hakuhusika kivyovyote katika shughuli za matanga, wala mazishi.

Bi Waithira, hata hivyo, alionyesha korti picha akiwa katika kaburi ambapo alikuwa akipanda maua kaburini na kudai kuwa yalikuwa mazishi ya marehemu. Mjomba wa Bi Wandia, Isaac Mugambi alieleza korti kuwa mke wa marehemu ambaye alifahamika ni mamake Wandia pekee, ambaye alifariki kitambo.

Bi Waithira alijaribu kujitetea akisema kuwa walifunga ndoa na marehemu kitamaduni, japo alisema kuwa hana uhakika ikiwa alilipiwa mahari.

Jaji Muchemi alitupilia mbali ushahidi wa picha uliotolewa na Bi Waithira kuonyesha kuwa walikuwa wameoana na marehemu, japo alikiri kuwa picha zenyewe zilionyesha kuwa kulikuwa na uhusiano wa karibu baina yake na marehemu.

Korti iliambiwa kuwa marehemu alianza kuishi na Bi Waithira mnamo 1997, miaka michache baada ya mkewe wa kwanza kufariki. Bw Njagi, hata hivyo, alifariki miaka mitano baadaye na hawakuwa na mtoto pamoja.

Korti iliamua kuwa hakuna ndoa iliyowahi kufungwa baina ya marehemu na Bi Waithira, japo ikasema kuwa wawili hao walikaa pamoja kwa muda, hali ambayo inaweza kudhaniwa kuwa ndoa.

Jaji aliendelea kutoa uamuzi kuwa kutokana na hali yao kukaa pamoja kwa muda huo, Bi Waithira anaweza kutajwa kuwa mjane wa marehemu, na kuwa kwa msingi huo anaweza kuruhusiwa kurithi mali. Aliamrisha Bi Waithira na Bi Wandia wote waruhusiwe kumiliki mali ya marehemu.