Michezo

Fenerbahce pazuri kutwaa huduma za Wanyama

July 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara 19 wa Ligi Kuu ya Uturuki, Fenerbahce wameingia sokoni kutafuta kiungo mkabaji na sasa wanasemekana wanamezea mate Mkenya Victor Wanyama.

Kwa mujibu wa tovuti ya Sport Witness, nyota huyu wa zamani wa Southampton huenda akahama Tottenham Hotspur katika kipindi hiki cha uhamisho kufuatia kuwasili kwa Mfaransa Tanguy Ndombele kutoka Lyon mapema mwezi huu wa Julai.

“Baada ya kuachana na kiungo Mehmet Topal mapema katika kipindi hiki cha uhamisho, Fenerbahce inatafuta kiungo mzoefu, huku mchezaji huyo wa Tottenham (Wanyama) akisemekana ni mmoja wa wachezaji klabu hiyo kutoka jijini Istanbul inaangalia,” tovuti hiyo imesema Jumatatu.

Imefichua kuwa kiungo Luiz Gustavo yuko juu ya orodha hiyo na kuwa mazungumzo kati ya klabu yake ya Marseille na Fenerbahce yamekuwa yakiendelea.

Hata hivyo, tovuti hiyo imenukuu gazeti la Sabah nchini Uturuki likisema kuwa Fenerbahce itamtafuta Wanyama isipopata Mbrazil huyo aliyepata umaarufu akichezea miamba wa Ujerumani, Bayern Munich kati ya mwaka 2011 na 2013.

Mkurugenzi wa michezo wa Fenerbahce, Damien Comolli anasemekana anatumai kusaini Wanyama kwa kutumia uhusiano wake wa karibu na Tottenham alikofanya kazi miaka michache iliyopita.

“Inasemekana kuwa Tottenham inatafuta kupata Sh1.1 bilioni kwa kuuza Wanyama aliyegonga umri wa miaka 28 mnamo Juni 25, 2019, na mazungumzo kati ya klabu hizi mbili yanatarajiwa kufanywa katika siku chache zijazo,” Sport Witness imesema. Kandarasi ya nahodha huyu wa timu ya taifa ya Kenya uwanjani Tottenham itatamatika Juni mwaka 2021.

Ripoti za Wanyama kuhusishwa na Fenerbahce zinawasili siku chache baada ya tetesi kuwa West Ham United pia iko tayari kumpa makao mapya ikipoteza Pedro Obiang kwa klabu nyingine.